Korea Kaskazini yaionya Marekani kwa miamala yake mibaya katika mazungumzo
(last modified Wed, 29 Aug 2018 14:50:31 GMT )
Aug 29, 2018 14:50 UTC
  • Korea Kaskazini yaionya Marekani kwa miamala yake mibaya katika mazungumzo

Serikali ya Korea Kaskazini imewaonya viongozi wa Marekani juu ya uwezekano wa kuvunjika mazungumzo kati ya pande mbili, kufuatia hatua ya Washington ya kumzuia Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo Mike Pompeo kutembelea Pyongyang.

Kwa mujibu wa habari hiyo, hivi karibuni serikali ya Korea Kaskazini iliitumia barua ikulu ya White House ambayo ndani yake iliionya Marekani juu ya mienendo yake mibaya katika kutia dosari mazungumzo ya kutokomeza silaha za nyuklia katika eneo la Korea na kusisitiza kwamba, kuna uwezekano wa mazungumzo hayo yakavunjika. Marekani imekiri kupokea barua kutoka kwa serikali ya Pyongyang na kusema kuwa, madhumuni ya barua hiyo ya Korea Kaskazini yalikuwa mazito kiasi cha kuifanya serikali ya Marekani kuvunja safari ya Waziri wake wa Mambo ya Nje Mike Pompeo kwenda Pyongyang.

Siku ambayo Trump na Kim Jong-un walikutana nchini Singapore

Jumapili iliyopita gazeti rasmi la Korea Kaskazini la Rodong Sinmun liliishutumu Marekani kuwa haina mwamana na inafanya undumakuwili  katika siasa zake za kigeni. Lliandika kuwa, hatua ya Washington ya kuvunja safari ya Mike Pompeo kwenda Pyongyang, imechukuliwa kiunafiki na ni katika kutekeleza njama za kivita dhidi ya Korea Kaskazini. Itakumbukwa kuwa Ijumaa usiku, Rais wa Marekani Donald Trump alidai kwamba, mazungumzo ya kutokomezwa silaha katika Rasi ya Korea yanaenda mwendo wa kinyonga na ndio maana ameamua kufuta safari ya Waziri wake wa Mambo ya Nje kwenda Pyongyang. Hayo yanajiri katika hali ambayo tarehe 12 Juni mwaka huu viongozi wa nchi mbili hizo walikutana nchini Singapore na kutiliana saini makubaliano ambayo kwa mujibu wake Korea Kaskazini iliahidi kutokomeza silaha zake za nyuklia huku kwa upande wake Marekani ikiahidi kuidhaminia usalama nchini hiyo. Hata hivyo tangu wakati huo hadi hivi sasa, Marekani imekuwa ikiiwekea mashinikizo na vikwazo nchi hiyo ya Asia na imekuwa ikikanyaga waziwazi makubaliano hayo ya Singapore.

Tags