Uamuzi kwa manufaa ya Palestina; Paraguay yaurejesha ubalozi wake Tel Aviv
Luis Alberto Castiglioni Waziri wa Mambo ya Nje wa Paraguay amesema kuwa nchi hiyo itaurajesha ubalozi wake Tel Aviv kutoka Quds Tukufu.
Castiglioni amebainisha kuwa Paraguay inataka kusaidia kutambuliwa jitihada za kidiplomasia za kieneo kwa ajili ya kufikiwa amani ya kiadilifu na ya kudumu katika eneo la Mashariki ya Kati. Hatua hii inahesabiwa kuwa aina fulani ya kubadilishwa msimamo wa rais wa zamani wa Paraguay Horacio Cartes ambaye aliamua kuuhamishia ubalozi wa nchi hiyo huko Quds kutoka Tel Aviv.
Kwa upande wake Wizara ya Mambo ya Nje wa Palestina imetangaza kuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Palestina ndiye aliyemshawishi Rais mpya wa Paraguay abadili msimamo wake wa kuuhamishia ubalozi wa nchi yake katika mji wa Quds. Sambamba na kuchukuliwa hatua hii, utawala wa Kizayuni umemwita nyumbani balozi wake anayehudumu nchini Paraguay ili kufanya kile ilichokitaja kuwa ni mashauriano kuhusu uamuzi wa nchi hiyo wa kuurejesha ubalozi wake huko Tel Aviv kutoka katika mji wa Quds unaokaliwa kwa mabavu, na wakati huohuo kutishia kufunga ubalozi wake katika nchi hiyo ya Amerika ya Latini. Kabla ya hapo, katika fremu ya mpango kwa jina la "Muamala wa Karne" Rais Donald Trump wa Marekani tarehe Sita Disemba mwaka jana alitangaza mji wa Quds unaokaliwa kwa mabavu kuwa mji mkuu wa utawala bandia wa Israel; na kutangaza pia uamuzi wake wa kuhamishia ubalozi wa Marekani huko Quds. Serikali ya Marekani tarehe 14 Mei mwaka huu ulianza kutekeleza uamuzi huo.