Waislamu nchini India waandamana kuwatetea Waislamu wa China
Waislamu nchini India wamefanya maandamano kuiunga mkono jamii ya Waislamu wa Uighur wanaokandamizwa katika mkoa wa Xinjiang nchini China.
Maandamano hayo yamefanyika katika mji wa Mumbai, ambapo wameitaka serikali ya China kukomesha vitendo vya kamatakamata dhidi ya jamii ya wachache ya Waislamu wa Uighur katika mkoa huo. Katika fremu hiyo, hivi karibuni Umoja wa Mataifa ulitoa taarifa ukionyesha wasi wasi wake juu ya siasa za ukandamizaji zinazotekelezwa na serikali ya China katika kuamiliana na jamii ya Waislamu wa nchi hiyo. Inafaa kuashiria kuwa, serikali ya Beijing na kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi, imeanzisha vituo kadhaa katika mkoa wa Xinjiang ambavyo vimekuwa vikitumika katika kuwazuilia ndani yake Waislamu wa jamii hiyo.
Hii ni katika hali ambayo serikali ya China imetoa ripoti kadhaa zikipinga ripoti ya timu ya Umoja wa Mataifa iliyothibitisha kwamba karibu Waislamu wa Uighur milioni moja wanazuiliwa na maafisa usalama wa nchi hiyo. Hatua za kiusalama zimeongezeka katika miaka ya hivi karibuni ndani ya mkoa wa Xinjiang sambamba na kuanzishwa vituo vingi vya upekuzi vya polisi kwa ajili ya kufuatilia nyendo za wakazi wa mkoa huo ambao wengi wao ni Waislamu.