Kimbunga Mangkhut chaingia China, baada ya kuua 60 Ufilipino
https://parstoday.ir/sw/news/world-i48178-kimbunga_mangkhut_chaingia_china_baada_ya_kuua_60_ufilipino
Kimbunga kikali cha Mangkhut kimewasili nchini China baada ya kuua watu 60 kaskazini mwa Ufilipino.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 16, 2018 10:17 UTC
  • Kimbunga Mangkhut chaingia China, baada ya kuua 60 Ufilipino

Kimbunga kikali cha Mangkhut kimewasili nchini China baada ya kuua watu 60 kaskazini mwa Ufilipino.

Tufani hiyo inayohesabiwa kuwa kubwa zaidi mwaka huu imesababisha uharibifu mkubwa katika miji ya Hong Kong na Macau, ambapo watu 200 wamejeruhiwa, huku majengo marefu yakitikiswa.

Kadhalika kimbunga hicho kimesababisha uharibifu mkubwa katika mji wa pwani wa Jiangmen, mkoani Guangdong kusini mwa China. 

Kimbunga cha Mangkhut

Kimbunga hicho kikali ambacho kinasafiri kwa mwendo wa kasi kubwa wa kilomita 230 kwa sasa kimesomba boti na miti katika miji hiyo ya China mapema leo Jumapili.

Kabla ya kuwasili China, Kimbunga cha Mangkhut kiliua watu 59 katika miji ya Luzon na Baggao nchini Ufilipino. 

Mwaka jana, watu zaidi ya 200 waliaga dunia kutokana na kimbunga kilichosababisha mafuriko na maporomoko ya ardhi nchini Ufilipino.

Mwaka 2013, kimbunga kikali cha Haiyan kiliua zaidi ya watu elfu 8 huko Uflipino, nchi ambayo inashuhudia vimbunga zaidi ya 20 kila mwaka.