Roma wajiunga na walimwengu kulaani jinai za Saudia nchini Yemen
Kundi moja la wananchi wa Italia limekusanyika mbele ya ubalozi wa Saudi Arabia mjini Rome kulaani jinai za Aal Saud huko Yemen.
Kwa mujibu wa shirika la habari la IRIB, waandamanaji hao walikuwa wamebeba picha za raia na watoto wadogo wa Yemen waliouliwa kinyama na ukoo wa Aal Saud na kulalamikia kumya kinachoendelea kuoneshwa na nchi za Magharibi ikiwemo serikali ya Italia mbele ya jinai hizo.
Waandamanaji hao wameitaka serikali ya Italia iache kuiuzuia Saudi Arabia silaha na zana za kijeshi hususan mabomu.

Waandamanaji hao wamesema, kuiuzia silaha Saudi Arabia ni kinyume na katiba ya Italia kwani kwa mujibu wa sheria za nchi hiyo, wakati nchi inapotumia silaha kushambulia raia, basi Italia haina ruhusa ya kuiuzia silaha.
Uvamizi wa Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu nchini Yemen ambao unaendelea kwa baraka kamili za Marekani, Israel na madola kadhaa ya Ulaya, ulianza mwezi Machi 2015 na hadi hivi sasa umeshaua zaidi ya watu 14 elfu, kujeruhi makumi ya maelfu wengine na kuwafanya wakimbizi mamilioni ya raia wasio na hatia huko Yemen.
Uvamizi huo wa kikatili umeisababishia Yemen matatizo mengi makubwa hasa ya upungufu mkubwa wa madawa, chakula na mahitaji mengine ya lazima.
