Uturuki yawatia mbaroni wanajeshi 85 wa 'harakati ya Gulen'
Vyombo vya usalama nchini Uturuki vimewatia nguvuni wanajeshi 85 waliokuwa kazini kwa tuhuma za kuwa na ushirikiano na harakati ya Fethullah Gülen.
Duru za polisi zimearifu kuwa, wanajeshi hao wamekamatwa katika mji mkuu Ankara na mikoa mingine 15 katika pembe mbalimbali za nchi.
Habari zaidi zinasema kwamba, agizo la kukamatwa maafisa hao wa Kamandi ya Jeshi la Anga la Uturuki limetolewa na Mkuu wa Mashitaka ya Umma wa mji mkuu Ankara, na kwamba askari wengine 25 wangali wanasakwa.
Mapema mwezi huu, Mkuu wa Mashtaka wa mji wa Bursa ulioko magharibi mwa Uturuki aliiagiza polisi ya nchi hiyo kufanya operesheni ya kuwatia nguvuni watuhumiwa wengine 25 katika maeneo ya Gemlik, Kestel, Inegol na Karacabey.
Kwa mujibu wa maafisa wa serikali ya Ankara, zaidi ya watu laki mbili na 28 elfu wana uhusiano na kundi la Fethullah Gülen na wanaitakidi kwamba watu hao wamehusika moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja na jaribio lililofeli la mapinduzi ya kijeshi lililotokea Julai 15 mwaka 2016 dhidi ya serikali ya Rais Recep Tayyip Erdogan.
Baada ya kutokea jaribio hilo, makumi ya maelfu ya watu walitiwa mbaroni nchini Uturuki kwa tuhuma za kuwa na uhusiano na kundi la Gülen huku wafanyakazi wapatao laki moja na 20 elfu wakiachishwa kazi katika vitengo na idara mbalimbali za serikali.