Kufutwa mazungumzo ya kijeshi kati ya Marekani na China
Wizara ya Ulinzi ya China na katika jibu lake dhidi ya siasa za mabavu na kupenda kujitanua za Marekani, imefuta mazungumzo ya kijeshi na nchi hiyo baada ya kufuta mazungumzo ya kibiashara baina ya pande hizo mbili.
Mazungumzo hayo yalikuwa yamepangwa kufanyika siku za Jumatatu hadi Jumatano mjini Beijing. Kadhalika serikali ya China imemrejesha nyumbani kamanda wa Jeshi la Majini la nchi hiyo aliyekuwa safarini nchini Marekani kwa ajili ya kushiriki mkutano wa 23 wa kimataifa wa makamanda wa majeshi ya majini. Alkhamisi iliyopita Rais Donald Trump wa Marekani kutokana na hatua ya China ya kununua ngao ya makombora ya S-400 na ndege za kivita kutoka Russia, alichukua hatua kadhaa alizozitaja kuwa za kulitia adabu Jeshi la China. Wizara ya Mambo ya Nje ya China pia katika kulalamikia mwenendo wa Marekani wa kuzidisha vikwazo dhidi ya Beijing, ilimwita balozi wa Marekani nchini humo Terry Branstad na kumkabidhi rasmi malalamiko yake kuhusiana na vikwazo hivyo vya Washington.
Hatua hiyo ya Marekani inaonyesha kwamba, mgogoro katika uhusiano wa nchi mbili umeongezeka, kama ambavyo pia Marekani inakusudia kuwalenga washirika wa kiuchumi na kijeshi wa Beijing. Japokuwa kisingizio kinachotumiwa na Marekani katika kadhia hii ni kuzidisha vikwazo dhidi ya China, lakini ukweli ni kwamba Washington pia imeilenga Russia na inafanya jitihada kuibana nchi hiyo katika ngazi ya kijeshi. Aidha kushadidishwa vikwazo vya Marekani dhidi ya China kunaonyesha kwamba, Washington ina wasiwasi wa kuongezeka zaidi uwezo wa kiuchumi na kijeshi wa nchi hiyo ya Asia na kuwa nguvu kubwa duniani, na hata siasa za kuipandishia ushuru wa kibiashara Beijing pia hazikuweza kuzuia ustawi wa kiuchumi wa China. Katika uwanja huo, Steve Banne, mtaalamu wa masuala ya kisiasa wa Marekani anasema: "Marekani imeazimia kukabiliana na ustawi wa kiuchumi wa China kwa kuwa ndio nchi pekee katika mustakbali wa karibu itakayoshika hatamu za uchumi duniani. Kwa sababu hiyo vita vya kiuchumi dhidi ya China ni vita yenye umuhimu mkubwa kwa Marekani. Ni kwa sababu hiyo ndio maana Marekani imejikita katika suala hilo kwa nguvu zake zote. Iwapo Washington itaendelea kushindwa katika vita vyake hivyo, hatimaye katika kipindi cha miaka 10 ijayo, nchi hiyo itafikia nukta ambayo hakutakuwepo njia yoyote nyingine ya kuweza kuirejesha nyuma”, mwisho wa kunukuu.
Mbali na hayo ni kwamba, kuendelea ushirikiano wa kijeshi wa China na Russia ni jambo jingine linaloizidishia wasiwasi wa White House kuhusu kuimarika uhusiano huo na kadhalika pande zingine, suala ambalo kwa mtazamo wa Marekani, linaweza kutoa changamoto kubwa kwa Washington katika maeneo mengine ya dunia. Ingawa China, kupitia fremu ya uhusiano wa kijeshi wa pande mbili, ingali inanunua silaha kutoka Russia, lakini katika miaka ya hivi karibuni serikali ya Beijing imepiga hatua kubwa za ustawi katika uundaji silaha, suala ambalo nalo limezidi kuitia wahka serikali ya Marekani hasa kutokana na hatua ya China ya kujiunga na Russia. Katika uwanja huo, Lee Jieh, mtaalamu wa masuala ya majeshi ya majini wa China anasema: “Uwezo wa silaha, nguvu za kupambana na kwa ujumla uwezo mkubwa wa kuandaa na kutayarisha Jeshi la Ukombozi la China umeongezeka sana hususan baada ya gwaride la mwezi Septemba 2015.”
Vilevile sambamba na serikali ya Marekani kuzidisha vikwazo dhidi ya China kwa lengo la kuizuia nchi hiyo kununua silaha za kisasa kutoka Russia, pamoja na mambo mengine, hatua hiyo ya Washington inadhihirisha ongezeko la siasa za White House za kutaka kuingilia masuala ya ndan ya nchi nyingine. Kwa msingi huo, iwapo China na Russia ambazo ni wanachama muhimu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, hazitasimama imara kuzuia sera hizo za Marekani, huwenda hapo baadaye mahusiano ya Moscow na Beijing yakakumbwa na changamoto kubwa na matatizo zaidi kutoka Washington.