Beijing yaitahadharisha Washington ijiepushe kutumia vibaya suala la haki za binadamu
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China ameitaka Washington itazame upya matatizo makubwa ya haki za binadamu yanayoisibu Marekani na wakati huo huo iache kutumia vibaya suala hilo kwa ajili ya kuingia masuala ya ndani ya nchi nyingine.
Akijibu matamshi ya karibuni ya viongozi wa Marekani kuhusu kile walichodai ni hali mbaya ya uhuru na haki za binadamu, Lu Kang amesisitiza kuwa, Marekani ambayo yenyewe ina matatizo makubwa ya haki za binadamu na imejitoa katika Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa haina haki ya kukosoa hali ya haki za binadamu katika nchi nyingine. Vilevile ameitaka Marekani iache kuituhumu China kuwa inafanya ujasusi katika mitandao ya kijamii na hatua nyingine kama hizo za kuingilia masuala ya ndani ya nchi hiyo.
Marekani imekuwa ikitumia suala la haki za binadamu kama wenzo wa kuziwekea mashinikizo nchi nyingine duniani. Washington inatumia mbinu hiyo kwa ajili ya kuziwekea mashinikizo nchi nyingine na kulazimisha sera na siasa zake zinazokinzana na haki za binadamu. Hii ni katika hali ambayo ripoti za kila mwaka zinazotolewa na serikali ya China kuhusu ukiukaji wa haki za binadamu nchini Marekani zinaonyesha kuwa, nchi hiyo ni mkiukaji mkubwa wa haki za binadamu na kwa msingi huo inapasa kurekebisha siasa zake katika uwanja huo kabla ya kuzungumzia hali ya haki za bindamu katika nchi nyingine. China imekosoa ukiukaji wa haki za binadamu nchini Marekani kupitia ripoti yake ya karibuni na kulalamikia vikali kile kinachotajwa nchini humo kuwa "matatizo ya kutisha ya haki za binadamu." Ndani ya ripoti hiyo kumeashiriwa pia masuala kama ukandamizaji wa kuogofya unaofanywa na polisi ya Marekani dhidi ya raia, kufungwa jela idadi kubwa ya watu, ubaguzi na sera za kibaguzi za masuala ya fedha.
Ripoti hiyo iliyotolewa na serikali ya China kuhusu ukiukwaji wa haki za binadamu nchini Marekani imekosoa namna serikali ya Washington inavyojifanya kigezo na mizani ya kutoa hukumu kuhusu haki za binadamu katika nchi nyingine na kufumbia macho matatizo ya dosari zake katika uwanja huo. Ripoti hiyo imeashiria takwimu za makundi ya kutetea haki za raia na vyombo vya habari vya Marekani kuhusu kuvurugika uhusiano baina ya mbari na watu wa kamu tofauti za Marekani mwaka 2016 na kukosoa hali hiyo. Hali imeshika mbaya zaidi katika utawala wa Donald Trump.
Mkurugenzi wa shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch mjini Washington anasema: Katika zama hizi za utawala wa Rais Trump tunashuhudia mabadiliko na matukio mengi kuhusu jinsi Marekani inavyoamilina na kadhia ya haki za binadamu ndani na nje ya nchi hiyo, kiasi kwamba hadi sasa hakuna rais yoyote wa nchi hiyo aliyewahi kufedheheshwa kwa kiasi hiki baada ya kutoa hotuba katika jukwaa la kimataifa kuhusu haki za binadamu.
Ripoti hiyo ya serikali ya China kuhusu hali ya haki za binadamu nchini Marekani pia imesisitiza kuwa katika hali ambayo sauti za risasi zinaendelea kusikika masikioni mwa Wamarekani nyuma ya sanamu la Uhuru, kuongezeka vitendo vya ubaguzi na vilevile maonyesho ya kuchekesha ya uchaguzi wa nchi hiyo unaoathiriwa na siasa za fedha vinaonyesha kuwa suala la haki za binadamu nchini Marekani ni dhihaka na hadithi za ngano.
Kitendo cha polisi ya Marekani cha kuwaua Alton Sterling na Philando Castile Wamarekani wenye asilia ya Afrika ambao hawakuwa na silaha yoyote ni mfano wa wazi wa jinai zinazojiri Marekani kila uchao licha ya nchi hiyo kujinadi kuwa ni mtetezi mkubwa zidi wa haki za binadamu.