Oct 16, 2018 07:28 UTC
  • Tuhuma na maneno makali ya Trump dhidi ya China

Uhusiano wa Marekani na China umekumbwa na misukosuko na panda shuka mbalimbali baada ya kuingia madarakani Donald Trump huko Marekani. Washington na Beijing zinahitilafiana katika masuala mengi ya kisiasa, kibiashara, kiuchumi, kijeshi, kiusalama na kiistratijia.

Katika nyaraka zake za kiusalama na kijeshi kama ile ya stratijia ya usalama wa taifa; Marekani imeitaja China kuwa nchi mpinzani wake na ni dola linalopenda kufanya mapinduzi na kusisitiza kuwa itakabiliana na siasa na hatua zinazochukuliwa na nchi hiyo. 

Trump ameonekana kuchukua maamuzi na hatua za upande mmoja katika kuamialiana na masuala mbalimbali kimataifa ikiwemo China pamoja na Russia zikiwa kama wapinzani wake wakuu. Wakati huo huo Beijing imekosoa vikali hatua anazozichukua rais huyo wa Marekani kuhusu biashara ya kimataifa akidai kuwa eti ni kwa ajili ya kulinda uchumi. Radiamali hizo za wazi za China mkabala na hatua za kihasama za Marekani zimeipelekea Washington kutekeleza siasa za vitisho na kushadidisha mashinikizo dhidi ya Beijing siku baada ya siku. Hivi karibuni Donald Trump kwa mara nyingine tena aliituhumu China kuwa iliingilia uchaguzi wa rais wa mwaka 2016 nchini Marekani na kuitaja nchi hiyo kuwa ni hatari zaidi kuliko Russia.  

Akijibu swali la kwamba je Russia iliingilia uchaguzi huo wa rais wa 2016; Trump alisema: Kwa hakika nadhani kuwa China ni tatizo kubwa zaidi.   

Hilary Clinton, mgombea wa kiti cha urais aliyechuana na Donald Trump mwaka 2016 huko Marekani

Viongozi wa Marekani mara kadhaa wamekuwa wakiituhumu Russia kuwa iliingilia moja kwa moja uchaguzi huo wa 2016 huko Marekani na kimsingi kuidhinishwa na kutekelezwa sheria ya vikwazo ya CATSA dhidi ya Russia kumefanyika kwa kisingizio hicho hicho. Hii ni katika hali ambayo Trump mwenyewe ni mtuhumiwa katika suala hili. Wapinzani wa Trump hususan Wademocrati wamelizungumzia jambo hilo mara kadhaa kwamba timu ya uchaguzi ya Trump ilifanya vikao vya siri na Warusi ili kumdhoofisha Bi Hillary Clinton mgombea wa kiti cha urais katika uchaguzi huo wa mwaka 2016 na kwamba maajenti wa Russia pia walidukua tovuti ya chama cha Democrat. Hata hivyo Trump amepinga tuhuma hizo na inaonekana kuwa ili kuweza kuipa nguvu kadhia hii, Trump hivi sasa anafanya jitihada kwa mtindo mwingine kama wa kuitumbukiza China katika suala hili.  

Trump amekuwa akihoji kwa kusisitiza akisema: Je mnadhani kweli mimi niliiomba Russia inisaidie katika uchaguzi? Hao kamwe hawakuwa na wezo wa kunisaidia. Jambo hili ni la mzaha kwa hakika.  

Wakati huo huo viongozi wa serikali ya Marekani hivi karibuni waliinyoshea China kidole cha tuhuma ambapo Kirstjen Nielsen, Waziri wa Usalama wa Ndani wa Marekani alisema: China imeanzisha kampeni ambayo haijawahi kushuhudiwa kwa lengo la kutafuta kuungwa mkono na fikra za walio wengi nchini Marekani, hata hivyo Beijing bado haijashambulia mifumo ya uchaguzi ya Marekani. 

Kirstjen Nielsen, Waziri wa Usalama wa Ndani wa Marekani 
 

Inaonekana kuwa Washington ambayo imeitaja waziwazi China kuwa ni dola linalopenda kufanya mapinduzi na kuitambua nchi hiyo kama mpinzani wake mkuu wa kiuchumi na kisiasa duniani na adui wake wa kijeshi mashariki mwa Asia, hivi sasa inafanya njama za kuzidisha mashiniko kwa Beijing kupitia kuzusha tuhuma mpya dhidi ya China; ili kwa njia hiyo iweza kuilazimisha iafiki matakwa yake ya kibiashara, kiuchumi na kiistratijia.    

Tags