Mwanamke ashambulia wanafunzi wa shule ya chekechea kwa kisu China
https://parstoday.ir/sw/news/world-i49053-mwanamke_ashambulia_wanafunzi_wa_shule_ya_chekechea_kwa_kisu_china
Mwanamke aliyekuwa amejizatiti kwa kisu amevamia shule moja ya chekechea nchini China na kujeruhi watoto 14 miongoni mwa wanafunzi wa shule hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 26, 2018 10:27 UTC
  • Mwanamke ashambulia wanafunzi wa shule ya chekechea kwa kisu China

Mwanamke aliyekuwa amejizatiti kwa kisu amevamia shule moja ya chekechea nchini China na kujeruhi watoto 14 miongoni mwa wanafunzi wa shule hiyo.

Taarifa ya Polisi ya China imesema kuwa, mwanamke huyo aliyetambulika kwa jina moja la Liu mapema leo aliwashambuliwa wanafunzi hao wa chekechea walipokuwa wakirejea darasani baada ya somo la mazoezi, katika mji wa Chongqing, kusini magharibi mwa China.

Polisi imesema imeanzisha uchunguzi kubaini lengo la mwanamke huyo kuwachoma kisu watoto wadogo. Majeruhi wamepelekwa katika hospitali ya Chongqing.

Askari polisi nje ya shule ya chekechea iliyoshambuliwa

Visa hivi vya watu waliojizatiti kwa silaha kushambulia wanafunzi vimekuwa vikifanyika mara kwa mara nchini China. Aghalabu wavamizi hao hutumia kisu, kwani China ina sheria kali ya kudhibiti umiliki wa silaha za moto.

Septemba mwaka huu, China ilitoa hukumu ya kunyongwa dhidi ya mwanamume mmoja aliyeua wanafunzi tisa na kujeruhi wengine 11 kwa kisu katika shule moja ya upili mkoani Shaanxi.