Dick Black: Uhusiano wa Marekani na Saudia unaainishwa na fedha
Richard Hayden Black, Seneta wa chama cha Republican nchini Marekani amesema kuwa, uhusiano wa Marekani na Saudi Arabia hautegemei misingi ya matukufu ya kimaadili, bali unategemea maslahi ya kiuchumi.
Black ambaye ni seneta wa jimbo la Virginia nchini Marekani ameyasema hayo katika mahojiano na kanali ya televisheni ya al-Akhbariyah na kuongeza kuwa, akthari ya wajumbe wa kongresi nchini humo wanataka kuhitimishwa uungaji mkono wa Washington kwa Riyadh katika vita vya Yemen. Ameongeza kwamba, katika uhusiano wa nchi mbili hizo hakuna suala la kimaadili na kutetea matukufu ya kibinaadamu, bali suala kuu ni fedha na madaraka. Richard Hayden Black ameendelea kufafanua kuwa, baada ya mauaji dhidi ya Jamal Khashoggi, mwandishi habari mkosoaji wa utawala wa Aal-Saud, raia wa Marekani waliishinikiza Kongresi ya nchi hiyo wakiitaka kuchukua hatua kali dhidi ya Riyadh, ambapo katika kongresi kulijadiliwa mapendekezo makali yaliyotakiwa kuchukuliwa kuhusiana na suala hilo, hata hivyo kwa bahati mbaya misimamo rasmi na ya mwisho ya Washington imesimama juu ya msingi wa maslahi ya kiuchumi na nguvu ya fedha.
Seneta huyo wa jimbo la Virginia amesema kuwa iwapo Saudia isingekuwa tajiri, basi Marekani ingekuwa inaitazama nchi hiyo kwa jicho la uhalisia wake wa nchi iliyobakia nyuma na katili, lakini Saudia inafanya juhudi kubwa kwa kutumia fedha zake kuweza kusafisha sura yake. Baada ya kufichuliwa kuwa Mohammad Bin Salman, Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudia alihusika katika mauaji ya Jamal Khashoggi, Rais Donald Trump alionyesha kutoridhia suala hilo, hata hivyo hakuwa tayari kusimamisha mauzo ya silaha kwa Saudia.