Kharrazi: Kuwepo Marekani nchini Afghanistan kumezidisha matatizo ya kiusalama
Mkuu wa Baraza la Kistratejia la Uhusiano wa Nje la Iran amesema kuwa Marekani imezidisha tu matatizo ya kiuaslama kwa Afghanistan baada ya kuweko nchini humo kwa muda wa miaka 17.
Sayyid Kamal Kharrazi amekutana na kufanya mazungumzo na Lakhdar Brahimi aliyekuwa Mjumbe Maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa huko Afghanistan na Syria na kujadili masuala mbalimbali ya Afghanistan na migogoro ya Asia Magharibi. Mazungumzo hayo yamefanyika katika ubalozi wa Iran mjini Paris Ufaransa.
Kuhusu harakati za kundi la kigaidi la Daesh huko Afghanistan, Sayyid Kharazi amebainisha kuwa Marekani imezidisha matatizo kwa nchi hiyo kwa kulipatia mwanya mkubwa kundi hilo la kigaidi.

Akijibu wasiwasi wa Lakhdar Brahimi kuhusu kuwepo mgawanyiko kati ya Washia na Wasuni huko Iraq, Mkuu huyo wa Baraza la Kistratejia la Uhusiano wa Nje la Iran amesema: Kwa bahati mbaya uungaji mkono wa baadhi ya nchi za Kiarabu la eneo la Ghuba ya Uajemi katika kuyaimarisha makundi ya kigaidi huko Iraq na Syria umezidisha ufa baina ya wananchi wa Iraq, hata hivyo madhehebu mbili hizo za Kiislamu huko Iraq zimekurubiana pakubwa kutokana na miongozo ya marja na viongozi wa Kiiraqi na pia makundi ya wananchi.
Katika mazungumzo hayo, naye Lakhdar Brahimi ambaye ni afisa wa zamani wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa nchi wanachama wa umoja huo zina wasiwasi kuhusu hali ya mambo ya Mashariki ya Kati na kusahauliwa kadhia ya Palestina.