Marekani yatishia kuanzisha Vita Baridi dhidi ya China
Wakati mivutano ya kibiashara kati ya Marekani na China inazidi kupamba moto, Makamu wa Rais wa Marekani Mike Pence ameoinya China kuhusu uwezekano wa kutokea Vita Baridi baina ya pande mbili.
Kwa mujibu wa tovuti ya Washington Examiner, Mike Pence ametoa onyo hilo nchini Singapore pembeni ya kikao cha Jumuiya ya Mataifa ya Kusini Mashariki ya Asia (ASEAN) na kutangaza kuwa Marekani haitalegeza msimamo katika mzozo wa kibiashara uliozuka baina yake na China hata kama jambo hilo litasababisha kuzuka Vita Baridi (Cold War).
Makamu wa Rais wa Marekani amedai pia kwamba, nchi hiyo iko katika nafasi imara na imeshatoza ushuru wa forodha wenye thamani ya dola bilioni 250.
Pence ameongeza kuwa, rais wa Marekani Donald Trump amefungua mlango kwa ajili ya kufikia mwafaka na China, lakini mwafaka huo utaweza kufikiwa endapo tu Beijing itafanya mabadiliko makubwa yanayotakiwa na Washington na kwamba hiyo ni fursa bora kwa China ya kuepusha kutokea Vita Baridi kati yake na Marekani.
Marekani, hadi sasa imezitoza ushuru wa fordha bidhaa zinazoingizwa nchini humo kutoka China wenye thamani ya dola bilioni 250; nayo China imeziwekea ushuru wenye thamani ya dola bilioni 110 bidhaa za Marekani zinazoingizwa nchini humo.
Tangu alipokuwa kwenye kampeni za uchaguzi wa rais hadi sasa, Trump amedai mara kadhaa kuwa China haijafanyia uadilifu Marekani katika sekta ya biashara.../