Asean yakosoa mauaji ya Waislamu wa Rohingya nchini Myanmar
Nchi zinazoshiriki katika mkutano wa Jumuiya ya Nchi za Kusini Mashariki mwa Asia (ASEAN) zimeikosoa vikali serikali ya Myanmar kutokana na mauaji yanayofanyika nchini humo dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya.
Waziri Mkuu wa Malaysia, Mahathir Mohamad amesema katika mkutano wa 33 wa jumuiya ya ASEAN huko Singapore kwamba, Mshauri Mkuu wa Serikali ya Myanmar, Aung San Suu Kyi ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo amekuwa na mchango katika mauaji yanayofanywa na Mabudha wa nchi hiyo dhidi ya Waislamu.
Viongozi wa nchi zilizoshiriki katika mkutano wa ASEAN wamesema katika taarifa ya mwisho ya mkutano huo kwamba, wakimbizi wa Kiislamu wa Rohingya wanapaswa kurejea nchini kwao kwa heshima zote na kudhaminiwa usalama. Hata hivyo taarifa hiyo iliyolaani mauaji yanayofanywa huko Myanmar dhidi ya Waislamu inaonekana kuwa haikukidhi matakwa ya walimwengu yanayozitaka nchi na jumuiya mbalimbali za kimataifa kuchukua hatua kubwa zaidi na si kutosheka kwa kulaani na kutoa taarifa za kukosoa mauaji hayo kwa maneno matupu.

Ataa Nurul Islam Arakani ambaye ni mchambuzi wa masuala ya kisiasa huko Myanmar anasema: "Mgogoro wa Rohingya unazidi kuwa mkubwa zaidi siku baada ya siku tangu mwaka 2012 na nchi na jumuiya za kimataifa hazijatekeleza majukumu yao ipasavyo kuhusu suala hilo. Nchi na jumuiya hizo zimetosheka kutoa maoni na taarifa tupu ambazo hazina taathira yoyote katika kusitisha mashaka na masaibu ya Waislamu wa Rohingya."
Tangu tarehe 25 Agosti mwaka 2017 pekee hadi sasa zaidi ya Waislamu elfu sita wameuawa katika jimbo la Rakhine, elfu nane wamejeruhiwa na zaidi ya milioni moja wamelazimika kukimbia makazi yao kutokana na ukatili unaofanywa na jeshi la Myanmar likishirikiana na Mabudha wenye misimamo mikali.
Kati ya nchi zote wanachama wa jumuiya ya ASEAN, Malaysia ndiyo iliyoko mshtari wa mbele katika kukosoa jinai na mauaji yanayoendelea kufanyika nchini Myanmar dhidi ya Waislamu. Malaysia imekuwa ikisisitiza udharura wa kukomeshwa mauaji hayo na kuishinikiza zaidi serikali ya Myanmar. Vilevile ndiyo nchi pekee katika jumuiya hiyo ambayo imeyatambua jinai hiyo kuwa ni mauaji ya kimbari.

Nchi wanachama wa ASEAN na jamii ya kimataifa kwa ujumla zimetoa wito wa kusitishwa uhalifu mkubwa unaofanyika nchini Myanmar na kuishinikiza serikali ya nchi hiyo kwa kutumia nyenzo zote zinazowezekana. Katika uwanja huo suala la kusimamishwa uanachama wa Myanmar katika jumuiya ya ASEAN na kuwekewa vikwazo vya kiuchumi na kijeshi vinatajwa kuwa vinaweza kuwa baadhi ya njia zinazoweza kusaidia jitihada za kukomeshwa mgogoro wa Rohingya na hatimaye kukomesha maafa na mashaka ya Waislamu wa jamii hiyo.
Alaa kulli hal, sisitizo la taarifa ya mwisho ya mkutano wa 33 wa jumuiya ya ASEAN huko Singapore juu ya udharura wa kurejea wakimbizi wa Rohingya nchini Myanmar na kudhaminiwa usalama linadhihirisha wasiwasi mkubwa wa jamii ya kimataifa kuhusu mustakbali usiojulikana na unaotia wasiwasi wa wakimbizi hao. Hasa ikitiliwa maana kwamba, ripota maalumu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa ameitaka Bangladesh kutisha mipango ya kuwarejesha maelfu ya Waislamu wa Rohingya nchini Myanmar.

Mkurugenzi wa shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch katika masuala ya wakimbizi, Bill Frelick anasema: "Kazi nyingi zinapaswa kufanyika kabla ya kuchukua hatua ya kuwarejesha wakimbizi wa Kiislamu wa Rohingya katika jimbo la Rakhine, na jamii ya kimataifa inalazimika kuweka wazi kwamba, haiwezekani kuchukua hatua kama hiyo bila ya kuwepo usimamizi wa kimataifa. Mbali na hayo, wasimamizi wa kimataifa wanapaswa kwanza kudhamini haki za awali na za kimsingi za Waislamu wa Rohingya ikiwa ni pamoja na kuwadhaminia usalama na amani na kuondoa kabisa dhana kwamba wakimbizi hao wanapelekwa tena kwenye kambi za wakimbizi nchini kwao."
Baada ya mwaka mmoja sasa wa wimbi jipya la ukatili na mauaji ya Mabudha na jeshi la Myanmar dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya, walimwengu wanatarajia kwamba, Umoja wa Mataifa na jumuiya nyingine kubwa za kikanda na kimataifa zitachukua hatua kubwa zaidi ya kusitisha maafa hayo ambayo yanatajwa kuwa ni miongoni mwa jinai kubwa zaidi duniani katika karne ya sasa.