Jumapili, 31 Agosti, 2025
Leo ni Jumapili tarehe 7 Mfunguo Sita Rabiul-Awwal 1447 Hijria mwafaka na 31Agosti 2025.
Katika siku kama ya leo miaka 1104 iliyopita Ali bin Muhammad Tanukhi alimu, mwandishi na malenga mashuhuri wa karne ya nne Hijria aliaga dunia huko katika mji wa Basra, kusini mwa Iraq akiwa na umri wa miaka 64. Ali Tanukhi alizaliwa huko Antakia mashariki mwa Uturuki ya leo na akiwa kijana alielekea Baghdad na kuasisi makazi yake. Ali bin Muhammad Tanukhi alikuwa mahiri katika lugha na fasihi ya Kiarabu na kuwa miongoni mwa malenga mashuhuri wa zama hizo. Mbali na kutunga diwani yake ya mashairi ambayo imebaki kama kumbukumbu hadi hii leo, Tanukhi aliandika pia vitabu mbalimbali kimojawapo kikiwa ni kile alichokipa jina la al Arudh. ***

Miaka 204 iliyopita katika siku kama hii, yaani tarehe 31 Agosti 1821, alizaliwa mwanafizikia na tabibu mashuhuri Hermann Ludwig Ferdinand von Helmholtz katika mji wa Potsdam nchini Ujerumani. Msomi huyo alihitimu masomo yake katika fani ya utabibu na mnamo mwaka 1849 alifikia daraja ya uprofesa wa fiziolojia na fizikia katika vyuo vikuu vya Berlin na Heidelberg. Japokuwa Helmholtz alitambulika zaidi kama mwanafizikia, mwanabiolojia na tabibu, lakini alikuwa mtaalamu wa hisabati na falsafa pia. Mwanafizikia huyo alitoa mchango mkubwa sana katika fani za electrodynamics na chemical thermodynamics. Katika uga wa falsafa, Herman Ludwig Ferdinand Von Helmholtz ndiye mwasisi wa falsafa ya sayansi, ambayo ni tawi la falsafa linalohusika na misingi, njia na matumizi ya sayansi. Msomi huyo alifariki dunia mwaka 1894 akiwa na umri wa miaka 73. ***

Miaka 68 iliyopita, yaani tarehe 31 Agosti 1957 nchi ya Malaysia iliyoko mashariki ya bara la Asia ilipata uhuru wake kutoka kwa Uingereza. Watu wa Malaysia walianza kidogo kidogo kuingia katika Uislamu katika karne ya 13 Miladia. Ushawishi wa Wazungu kutoka Ulaya katika nchi hiyo ulianza mwanzoni mwa karne ya 16 alipowasili nchini humo baharia wa Kireno Afonso de Albuquerque. Mnamo karne ya 17 Uholanzi iliikalia na kuitawala Malaysia; na ulipofika mwaka 1824 na kufuatia mkataba wa makubaliano yaliyofikiwa baina ya Uingereza na Uholanzi, Malaysia ikatawaliwa na Uingereza na Indonesia ikakabidhiwa Uholanzi. Uingereza iliendelea kuitawala Malaysia hadi ilipopata uhuru wake katika siku kama ya leo. ***

Katika siku kama ya leo miaka 63 iliyopita, nchi ya Trinidad na Tobago ilipata uhuru kutoka kwa Uingereza, na siku hii inajulikana kama siku ya kitaifa ya nchini humo. Nchi hiyo hapo awali ilikuwa koloni la Uhispania, lakini ilikabidhiwa kwa Uingereza mnamo 1802. Jamhuri ya Trinidad na Tobago, yenye eneo la kilomita za mraba 5,128, iko kaskazini mwa Bahari ya Atlantiki ya Amerika Kusini. ***

Miaka 47 iliyopita katika siku kama hii ya leo, yaani tarehe 31 Agosti 1978, Imamu Musa Sadr alitoweka katika mazingira ya kutatanisha alipokuwa safarini nchini Libya. Imamu Musa Sadr alizaliwa tarehe 4 Juni mwaka 1928 katika mji wa Qum nchini Iran. Baada ya kumaliza masomo, mwaka 1959 alielekea Lebanon. Wakati huo, Waislamu wa nchi hiyo walikuwa na hali mbaya sana kijamii, kisiasa na kiuchumi. Kutokana na hali hiyo, Imamu Musa Sadr alichukua hatua kadhaa za msingi ili kuboresha hali zao na ndipo alipobuni taasisi ya kushughulikia masuala ya Waislamu wa Kishia iitwayo "Baraza Kuu la Mashia wa Lebanon". Taasisi hiyo ilipitishwa katika bunge la nchi hiyo na yeye akachaguliwa kuwa mkuu wake. Imamu Musa Sadr alikuwa pia akiunga mkono kikamilifu mapambano ya Wapalestina dhidi ya utawala haramu wa Kizayuni wa Israel; na kwa ajili hiyo akaanzisha "Harakatul-Mahrumin" ambayo ililenga kutetea haki za Waislamu wa Lebanon pia. Tangu Imamu Musa Sadr alipotoweka, zimefanyika jitihada nyingi na kubwa za kupata taarifa kuhusu hatima yake, lakini hadi sasa hazijazaa matunda. ***
