Makumi wauawa katika mripuko kwenye kiwanda cha kemikali China
https://parstoday.ir/sw/news/world-i49819-makumi_wauawa_katika_mripuko_kwenye_kiwanda_cha_kemikali_china
Kwa akali watu 22 wameripotiwa kupoteza maisha baada ya kutokea mripuko karibu na kiwanda cha kemikali katika mji wa Zhangjiakou, mkoani Hebei kaskazini mwa China.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 28, 2018 04:10 UTC
  • Makumi wauawa katika mripuko kwenye kiwanda cha kemikali China

Kwa akali watu 22 wameripotiwa kupoteza maisha baada ya kutokea mripuko karibu na kiwanda cha kemikali katika mji wa Zhangjiakou, mkoani Hebei kaskazini mwa China.

Shirika rasmi la habari la China la Xinhua limeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, mripuko huo ambao umetokea mapema leo pia umesababisha watu 22 kujeruhiwa huku magari zaidi ya 50 yakiteketea kwa moto na kubaki majivu.

Habari zinasema kuwa, Kiwanda cha Kemikali cha Hebei Shenghua ambacho kiko karibu na eneo la tukio kimefungwa na kwamba moto huo umeweza kudhibitiwa na timu ya wazimamoto.

Mji huo wa Zhangjiakou, ambao uko umbali wa kilomita 156 kaskazini mwa mji mkuu Beijing, unatazamiwa kuwa mwenyeji wa Michezo ya Olimpiki ya Msimu wa Baridi Kali ya mwaka 2022.

Mabaki ya kiwanda cha kuzalisha kemikali baada ya mripuko

Wananchi wa China wamekuwa wakikosoa vikali kutochukuliwa hatua za kuzuia majanga, huku visa vya mikasa ya aina hii viwandani vikiripotiwa kila uchao.

Itakumbukwa kuwa, Agosti mwaka 2015, watu 165 waliaga dunia katika mripuko mkubwa uliotokea katika ghala la kuhifadhi kemikali katika mji bandari wa Tianjin.