Mripuko wa fataki waua watu 8 kanisani nchini Mexico
Kwa akali watu wanane wamepoteza maisha na wengine wengi wamejeruhiwa baada ya kutokea mripuko wa fataki katika kanisa moja nchini Mexico.
Gabriel Bastarrachea, ofisa wa Idara ya Kupambana na Majanga katika jimbo la Queretaro amesema watoto wawili wa miaka 11 na 12 ni miongoni mwa watu waliouawa katika mripuko huo uliotokea katika Kanisa la San Jose katika mji wa Tequisquiapan, yapata kilomita 145 kaskazini magharibi mwa mji mkuu Mexico City.
Julai mwaka huu, watu zaidi ya 20 waliuawa katika miripuko kadhaa ya fataki iliyotokea katika mji wa Tultepec nchini Mexico.
Katika hatua nyingine, watu wanne wameuawa baada ya mtu aliyekuwa amejizatiti kwa bunduki kuwamiminia risasi waumini wa Kikristo waliokuwa wamekusayika katika kanisa moja la Kikatoliki nchini Brazil.

Habari zaidi zinasema kuwa, mtu huyo alijitoa uhai kwa kujifyatulia risasi kichwani baada ya kufanya shambulizi hilo jana Jumanne dhidi ya Kanisa la Katoliki la Campinas, karibu na jiji la Sao Paulo.
Watu zaidi ya 12 wamejeruhiwa katika shambulizi hilo linaloaminika kuwa la kigaidi.