Umoja wa Ulaya walaani ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni
Umoja wa Ulaya umetoa taarifa na kusema kuwa ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni unaoendelezwa na Israel kwa kujenga nyumba 2,191 katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan ni kinyume cha sheria.
Shirika la habari la IRIB limeinukuu ofisi ya Federic Mogherini, mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya ikisema jana Alkhamisi katika taarifa yake kwamba msimamo wa Umoja wa Ulaya wa kupinga ujenzi wa vitongoji vywa walowezi wa Kizayuni haujabadilika kwani kwa mujibu wa maazimio ya kimataifa, ujenzi huo ni kinyume cha sheria.
Taarifa hiyo ya Umoja wa Ulaya imeongeza kuwa, kuendelea Israel kujenga vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi inazowapora Wapalestina kunahatarisha juhudi za kuleta amani katika eneo hili.
Tofauti kabisa na Marekani ambayo hasa baada ya kuingia madarakani nchini humo rais wa hivi sasa, Donald Trump, imekuwa ikuunga mkono kikamilifu jinai zote za Israel, Umoja wa Ulaya kwa upande wake hauko hivyo bali mara kwa mara umekuwa ukichukua hatua za wazi za kupinga jinai za utawala wa Kizayuni kama vile kupora ardhi za Wapalestina na kujenga vitongoji vya walowezi wa Kizayuni.
Kwa muda mrefu sasa utawala wa Kizayuni umekuwa ukiteka ardhi za Wapalestina na kujenga vitongoji vya walowezi wa Kizayuni kwa lengo la kuvuruga muundo wa kijiografia na kijamii katika maeneo ya Wapalestina kwa uungaji mkono wa kila upande wa Marekani.
Tarehe 23 Disemba 2016, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipasisha azimio ambalo lengo lake ni kukomesha ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi za Wapalestina.