Uingereza yataka kuwa na nafasi kubwa zaidi katika uwanja wa kimataifa
https://parstoday.ir/sw/news/world-i50532-uingereza_yataka_kuwa_na_nafasi_kubwa_zaidi_katika_uwanja_wa_kimataifa
Uingereza ambayo inatambuliwa kuwa mwanachama muasi wa Umoja wa Ulaya Juni mwaka 2016 iliitisha kura ya maoni iliyowataka wananchi wa nchi hiyo wachague ama kuondoka au kubakia katika Umoja huo. Sasa baada ya wananchi kuchukua uamuzi wa kuondoka katika Umoja wa Ulaya maarufu kama Brexit imepangwa kuwa hadi mwezi Machi mwaka unaoanza kesho wa 2019 Uingereza itajitenga na Umoja wa Ulaya.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 31, 2018 02:49 UTC
  • Uingereza yataka kuwa na nafasi kubwa zaidi katika uwanja wa kimataifa

Uingereza ambayo inatambuliwa kuwa mwanachama muasi wa Umoja wa Ulaya Juni mwaka 2016 iliitisha kura ya maoni iliyowataka wananchi wa nchi hiyo wachague ama kuondoka au kubakia katika Umoja huo. Sasa baada ya wananchi kuchukua uamuzi wa kuondoka katika Umoja wa Ulaya maarufu kama Brexit imepangwa kuwa hadi mwezi Machi mwaka unaoanza kesho wa 2019 Uingereza itajitenga na Umoja wa Ulaya.

Inatazamiwa kuwa, utekelezaji kivitendo wa Brexit utaipatia nchi hiyo fursa ya kuchukua hatua mpya katika medani ya kimataifa na kujiunga na Marekani kwa kuzidisha nafasi na kuwepo kwake katika medani za kimataifa.

Katika uwanja huo Waziri wa Ulinzi wa Uingereza Gavin Williamson amesema kuwa, Brexit ni tukio kubwa na muhimu zaidi kwa nchi hiyo baada ya Vita vya Pili vya Dunia ambalo litaiwezesha London kuchukua nafasi yake inayostahiki duniani. Williamson anaamini kuwa, baada ya Brexit, Uingereza inaweza kuwa "mchezaji halisi" duniani kwa kuanzisha kambi mpya za kijeshi katika maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na katika maeneo ya Bahari ya Caribbean na Mashariki ya Mbali (Far East). Waziri wa Ulinzi wa Uingereza anasema: "Brexit itaiwezesha Uingereza kubadilisha siasa za muongo wa 1960 kuhusiana na kuondoka katika maeneo ya mashariki mwa Suez (East of Suez)."

Gavin Williamson, Waziri wa Ulinzi wa Uingereza 

Inaonekana kuwa, kutokana na kubadilika stratijia ya kijeshi ya Marekani kwa kujielekeza zaidi katika eneo la IndoPasific, sasa Uingereza imeazimia kufuata siasa za Washington na kutaka kuwa na nafasi muhimu zaidi katika kulinda maslahi ya Magharibi katika maeneo mbalimbali ya dunia kuanzia Bahari ya Caribbean, Singapore hadi Ghuba ya Uajemi. London daima imekuwa ikitangaza kuwa, ni mshirika wa kistratijia wa Marekani na hapana shaka kuwa, baada ya kujivua na sheria na vizuizi vya Umoja wa Ulaya itakuwa na uhuru mkubwa zaidi katika masuala ya kijeshi na kiusalama. Maafisa wa ngazi za juu wa chama tawala cha Conservative wanaamini kuwa, maslahi ya kitaifa ya Uingereza yameathiriwa na Umoja wa Ulaya kwa miongo kadhaa na kwamba sasa umewadia wakati wa kufuatilia tena maslahi hayo katika medani ya kimataifa kwa mutumia nguvu za kijeshi. Kwa maneno mengine tunaweza kusema kuwa, katika fremu ya harakati za kuhuisha siasa zake za kutaka kujipanua zaidi ambazo ziliwekwa kando mwishoni mwa muongo wa 196o kutokana na sababu mbalimbali, Uingereza inakusudia kuanzisha kambi za kijeshi katika maeneo mbalimbali ya dunia na kuwa "mchezaji" halisi katika medani ya kimataifa. Maafisa wa serikali ya Kihafidhina ya London wanaamini kuwa, nafasi na turathi ya Uingereza imedunishwa duniani na ili kuweza kuhuisha nafasi hiyo kuna ulazima wa kuhuishwa siasa za kutuma majeshi ya nchi hiyo katika maeneo mbalimbali ya dunia.

Waziri wa Ulinzi wa Uingereza anadai kuwa, Australia, Canada, New Zealand, nchi za kanda ya Caribbean na nchi za Afrika zinaitegemea nchi hiyo katika uongozi wa kimaadili, kijeshi na uongozi wa masuala ya dunia. Hata hivyo haijulikani maafisa wa Uingereza wametegemea kitu gani katika kutoa madai kama haya yasiyo na msingi. Inapasa pia kujua kwamba, mipango ya Uingereza ya kuzidisha uwepo wa majeshi yake katika maeneo ya kistratijia ya dunia si jambo jipya; na kupanuliwa kituo cha jeshi la majini la Uingereza katika nchi ndogo ya Bahrain kumefanyika katika mkondo huo huo. Baada ya kufunguliwa kituo hicho mwaka huu wa 2018, kwa mara ya kwanza kabisa tangu majeshi ya Uingereza yalipoondoka katika Ghuba ya Uajemi katika muongo wa 1970, jeshi la majini la nchi hiyo limeweza kurejea tena katika eneo la Ghuba ya Uajemi na kutengeneza makazi yake ya kudumu katika eneo hilo. Lengo la kuanzishwa kambi ya kudumu ya Uingereza huko Bahrain ni kurejea London katika stratijia zake za miaka ya nyuma yaani kuwepo maeneo ya “mashafiki mwa Suez”. Waziri wa Fedha wa Uingereza Philip Hammond aliwahi kusema kuwa: Lengo la kuanzishwa kituo cha jeshi la majini cha kudumu nchini Bahrain ni kurejea katika stratijia ya ‘East of Suez’, lakini katika fremu ya stratijia kubwa na pana zaidi.”

Meli za kivita za jeshi la majini la Uingereza katika kituo chake cha kudumu nchini Bahrain

Katika kipindi si kirefu kijacho jeshi la majini la Uingereza limepanga kutuma manuwari zake mpya za kijeshi zikiwemo zile zenye uwezo wa kubeba ndege, katika eneo la Ghuba ya Uajemi; na hapana shaka kuwa, suala hilo haliwezi kuwa na manufaa kwa amani na usalama wa eneo hilo nyeti. Kutumwa kwa manuwari hizo za kijeshi Ghuba ya Uajemi ni suala linalovuruga amani na kuchochea machafuko. London imekuwa ikiituhumu Iran kuwa imeanzisha mashindano ya silaha katika eneo hilo lakini inaonekna kuwa, hatua yake ya kuzidisha majeshi katika Ghuba ya Uajemi itazidisha pia mivutano na ukosefu wa amani katika eneo hilo la kistratijia.