Trump: Vikwazo dhidi ya Korea Kaskazini vitaendelea kutekelezwa
(last modified Mon, 07 Jan 2019 04:29:35 GMT )
Jan 07, 2019 04:29 UTC
  • Trump: Vikwazo dhidi ya Korea Kaskazini vitaendelea kutekelezwa

Rais Donald Trump wa Marekani amesisitiza juu ya kuendelea kutekelezwa kikamilifu vikwazo vya nchi yake dhidi ya Korea Kaskazini na amesema kuwa, vikwazo hivyo vitaendelea kuwepo.

Katika matamshi yake ya undumakuwili, Trump ameashiria kwamba mazungumzo kati ya Washington na Pyongyang yanaendelea kwa namna chanya, lakini madamu Washington haijapata ushahidi wenye taathira chanya kwa ajili ya kuiondolea Korea Kaskazini vikwazo, basi vikwazo hivyo vitaendelea kuwepo. Trump anasisitizia kuendelezwa vikwazo dhidi ya serikali ya Pyongyang katika hali ambayo, Kim Jong-un, Kiongozi wa Korea Kaskazini alikutana na rais huyo wa Marekani tarehe 12 Juni mwaka jana 2018 nchini Singapore na kutiliana saini makubaliano ambayo kwa mujibu wake, Pyongyang ilitakiwa kuangamiza kikamilifu silaha zake za nyuklia, huku kwa upande wake Marekani nayo ikitakiwa kuidhaminia usalama nchi hiyo ya Asia.

Trump alipokutana na Kim Jong-un tarehe 12 Juni nchini Singapore

Hata hivyo siku chache baada ya mkutano huo, rais wa Marekani na katika hali isiyotarajiwa alitia saini hati ya kurefushwa kwa kipindi cha mwaka mmoja zaidi, vikwazo vya kiuchumi dhidi ya Pyongyang. Licha ya serikali ya Korea Kaskazini kutekeleza hatua muhimu kwa ajili ya kupatikana usalama katika eneo la Rasi ya Korea ikiwemo kuharibu maeneo yake ya kufanyia majaribio ya silaha za nyuklia, lakini Marekani bado haijatekeleza ahadi zake ilizozitoa katika makubaliano ya tarehe 12 Juni mwaka jana, suala ambalo limekuwa likilalamikiwa na serikali ya Pyongyang.

Tags