Pyongyang yajibu mapigo, yavurumisha makombora baharini
https://parstoday.ir/sw/news/world-i123734
Korea Kaskazini imevurumisha makombora kadhaa ya balestiki baharini leo Jumatatu, saa chache baada ya wanajeshi wa Korea Kusini na Marekani kuanza mazoezi makubwa ya kijeshi ya kila mwaka ya pamoja, ambayo Pyongyang inayatazama kama majaribio ya uvamizi.
(last modified 2025-03-10T11:22:34+00:00 )
Mar 10, 2025 11:22 UTC
  • Pyongyang yajibu mapigo, yavurumisha makombora baharini

Korea Kaskazini imevurumisha makombora kadhaa ya balestiki baharini leo Jumatatu, saa chache baada ya wanajeshi wa Korea Kusini na Marekani kuanza mazoezi makubwa ya kijeshi ya kila mwaka ya pamoja, ambayo Pyongyang inayatazama kama majaribio ya uvamizi.

Wakuu wa Majeshi wa Korea Kusini wamesema kurushwa makombora hayo, ambalo ni tukio la tano la kuvurumishwa makombora nchini Korea Kaskazini mwaka huu, liligunduliwa kutoka mkoa wa Hwanghae Kaskazini lakini hawakutoa maelezo zaidi kama vile umbali wa kuruka makombora hayo.

Taarifa ya wakuu hao wa majeshi imesema Korea Kusini imeimarisha mkao wake wa ufuatiliaji na inashirikiana kwa karibu na Marekani katika hilo.

Mapema Jumatatu, wanajeshi wa Korea Kusini na Marekani walianza mazoezi yao ya pamoja ya kijeshi ya kila mwaka, ambayo yamepangwa kuendelea kwa siku 11.

Luteka hiyo ya 'Kamandi la Ngao ya Uhuru' imeanza baada ya wanajeshi wa Korea Kusini na Marekani kusitisha mazoezi ya kufyatua risasi hai, huku Seoul ikichunguza jinsi ndege zake mbili za kivita zilipiga mabomu kimakosa eneo la raia wakati wa maandalizi ya mazoezi wiki iliyopita.

Kuanza kwa maneva hayo kulilaaniwa na Korea Kaskazini, ambayo ilitoa taarifa ikiyataja mazoezi hayo kuwa "kitendo hatari cha uchochezi" ambacho kinaongeza hatari za migogoro ya kijeshi katika eneo.

Takriban watu 30 walijeruhiwa, wawili kati yao vibaya, wakati ndege mbili za kivita za Korea Kusini aina ya KF-16 zilivurumisha kimakosa mabomu manane ya MK-82 kwenye eneo la raia huko Pocheon, mji ulio karibu na mpaka wa Korea Kaskazini, siku ya Alkhamisi.