Russia: Marekani inabeba dhima ya hatima ya mkataba wa INF
https://parstoday.ir/sw/news/world-i50944-russia_marekani_inabeba_dhima_ya_hatima_ya_mkataba_wa_inf
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amesema kuwa Marekani ndiyo inayopaswa kubeba dhima ya hatima ya Mkataba wa Silaha za Nyuklia za Masafa ya Kati, (INF)
(last modified 2026-04-19T09:26:01+00:00 )
Jan 18, 2019 00:22 UTC
  • Russia: Marekani inabeba dhima ya hatima ya mkataba wa INF

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amesema kuwa Marekani ndiyo inayopaswa kubeba dhima ya hatima ya Mkataba wa Silaha za Nyuklia za Masafa ya Kati, (INF)

Sergei Ryabkov ameliambia shirika la habari la Interfax kwamba, maafisa wa serikali ya Russia wamewaeleza wenzao wa Marekani azma na utayarifu wa serikali ya Moscow wa kudumisha mazungumzo kuhusu Mkataba wa Silaha za Nyuklia za Masafa ya Kati (INF) wakati na mahala popote. 

Sergei Ryabkov ameongeza kuwa, timu ya Russia katika mazungumzo ya pande mbili yaliyofanyika Jumanne iliyopita mjini Geneva ilitoa pendekezo la kuchukuliwa hatua za kuweka wazi masuala yote na kuondoa wasiwasi kuhusu utekelezaji wa mkataba huo lakini matokeo ya mazungumzo hayo yameonyesha kwamba, Washington haitaki kutazama upya uamuzi wake wa kujiondoa katika mkataba huo.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amesema kuwa, kutokana na hali hiyo Marekani ndiyo inayobeba dhima ya hatima ya mkataba huo muhimu wa kudhibiti silaha za nyuklia za masafa ya kati.

Aliyekuwa Kiongozi wa Urusi ya zamani (USSR) Mikhail Gorbachev (kushoto) na rais wa wakati huo wa Marekani Ronald Reagan wakisaini mkataba wa INF

Makubaliano ya pande mbili ya kutokomeza Silaha za Nyuklia za Masafa ya Kati (INF) yalisainiwa mwaka 1987 na viongozi wa wakati huo wa Marekani na Shirikisho la Kisovieti la Urusi ya zamani na kutajwa kama hatua muhimu ya kuondoa hali ya mivutano katika enzi hizo za Vita Baridi.