Kusajiliwa kanali ya kifedha ya Ulaya; hatua iliyochelewa lakini inayotia matumaini
(last modified Fri, 01 Feb 2019 12:55:42 GMT )
Feb 01, 2019 12:55 UTC
  • Kusajiliwa kanali ya kifedha ya Ulaya; hatua iliyochelewa lakini inayotia matumaini

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amekaribisha kuzinduliwa mfumo maalumu wa kifedha wa nchi za Ulaya unaolenga kudumisha ushirikiano wa kiuchumi na Iran, ikiwa ni hatua ya kwanza iliyochukuliwa na nchi hizo kuhusiana na mapatano ya nyuklia ya Iran yanayojulikana kama JCPOA.

Akizungumzia suala hilo siku ya Alkhamisi, Abbas Araqchi ameeleza matumaini yake kwamba mfumo huo wa kifedha utatekelezwa kikamilifu, hautakuwa na kasoro na kujumuisha bidhaa zote za kibiashara na kiuchumi. Amesema: Mfumo wa kifedha wa Ulaya utakuwa na manufaa kamili kwa Iran pale utakaporuhusu kufikiwa nchi na mashirika mengine yasiyokuwa ya Ulaya.

Karibu miezi 9 baada ya kujiondoa Marekani katika mapatano ya nyuklia kati ya nchi sita kuu za dunia na Iran yanayojulikana kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji, JCPOA, na kuanzishwa tena vikwazo vya Washington dhidi ya Tehran, hatimaye nchi za Ujerumani, Ufaransa na uingereza zimeanzisha mfumo maalumu wa kifedha usiotumia sarafu ya dola kwa ajili ya kurahisisha mabadilishano ya kibiashara na kiuchumi na Iran na wakati huohuo kukwepa vikwazo vya Marekani. Mfumo huo wa kifedha unaojulikana kama INSTEX unakusudia kulinda manufaa ya kiuchumi ya mapatano ya JCPOA kwa maslahi ya Iran. Katika hatua ya kwanza, kanali hiyo ya kifedha itashughulikia bidhaa ambazo hazijawekewa vikwazo kama vyakula na madawa ili njia maalumu iweze kupatikana kwa ajili ya kutolewa malipo. Katika hatua ya pili kanali hiyo ya kifedha ya Ulaya itajumuisha bidhaa zilizowekewa vikwazo. Baada ya kujiondoa katika mapatano ya JCPOA, Marekani ilianza kutekeleza tena vikwazo dhidi ya Iran katika hatua mbili ambapo mafuta na miamala ya kibenki iliathirika na vikwazo hivyo.

Ushirikiano wa Ulaya na Iran

Lengo la hatua hiyo ya Marekani lilikuwa ni kutoa mashinikizo ya kiuchumi dhidi ya Iran na kufutilia mbali maslahi ya kiuchumi ya mapatano ya JCPOA kwa madhara ya serikali ya Tehran. Kwa msingi huo iwapo katika hatua ya pili nchi za Ulaya hazitajumuisha bidhaa zilizowekewa vikwazo katika kanali hiyo ya INSTEX wala kuyashawishi mashirika yao yafanye biashara na Iran, ni wazi kuwa kanali hiyo haitakuwa na umuhimu wowote katika kusaidia kukwepa vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran. Mpango huo wa kifedha uliozunduliwa Alkhamisi huko Bucharest mji mkuu wa Romania, bado una matatizo mengi ya kiufundi ambayo yanapaswa kutatuliwa. Kuhusiana na suala hilo, Reza Najafi, mkurugenzi mkuu wa kitengo cha Amani na Usalama katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran anasema: Kuzinduliwa kwa kanali ya kifedha ya Ulaya na Iran ni hatua ya mwanzo iliyochukuliwa na watu wa Ulaya kwa ajili ya kuunga mkono mapatano ya JCPOA, hatua ambayo inapaswa kutekelezwa kivitendo. Kwa vyovyote vile hatua hiyo iliyochukuliwa na Ulaya ambayo inaamini kwamba mapatano ya JCPOA yanapaswa kulindwa, ni hatua chanya. Wakati huohuo Federica Mogherini, Mkuu wa Siasa za Kigeni wa Umoja wa Ulaya amesema sambamba na kuzinduliwa kwa kanali hiyo maalumu ya kifedha: Ulaya inaunga mkono kikamilifu utekelezaji wa JCPOA.

Mawaziriwa wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, Uingereza na Ujerumani wakizungumzia suala la INSTEX Bucharest, Romania

Mapatano hayo ambayo ni matunda ya juhudi za kimataifa, yana umuhimu mkubwa kwa itibari ya Umoja wa Ulaya na ndio maana ukawa unayaunga mkono kwa nguvu zake zote za kisiasa. Pamoja na hayo mapatano hayo hayapaswi kuungwa mkono kisiasa tu bali yanahitajia uungaji mkono wa pande zote kisiasa na kiuchumi. Mashirika ya Ulaya yanapaswa kushawishiwa yajishughulishe kibiashara chini ya mfumo huo wa kifedha bila kuhofia kuadhibiwa na Marekani. Kufikiwa lengo hilo bila shaka kunahitajia juhudi zaidi za nchi za Ulaya, ambapo hata hazipasi kusita kulipa gharama ya kulinda mapatano ya JCPOA. Kwa kutilia maanani upinzani mkali wa Marekani juu ya kuzinduliwa kanali hiyo mpya ya kifedha kwa maslahi ya Iran, kuna uwezekano wa kudhihiri makabiliano na changamoto kubwa kati ya Washington na Ulaya kuhusiana na utekelezaji wa mfumo huo wa kifedha. Pamoja na hayo shirika la Bloomberg linasema katika ukurasa wake wa mtandaoni kwamba: Kuanzishwa kwa kanali ya kusaidia mabadilishano ya kifedha na Iran ni nukta muhimu sana inayoonyesha juhudi za Ulaya za kukabiliana na nguvu ya kiuchumi ya Marekani.

Tags