Russia yajibu mapigo baada ya Marekani kujiondoa INF
-
Vladimir Putin
Rais Vladimir Putin wa Russia ametangaza kuindoa Russia kwa muda katika mkataba wa Silaha za Nyuklia za Masafa ya Kati (INF), baada ya Marekani kufanya hivyo jana Ijumaa.
Sambamba na kutangaza uamuzi huo hii leo pambizoni mwa mawaziri wa ulinzi na mambo ya nje wa nchi hiyo, Rais Putin ameagiza uundwaji wa makombora ya kisasa yakiwemo ya (supersonic) kama radiamali kwa hatua hiyo ya Marekani.
Hata hivyo amesisitiza kuwa, Russia haitaki kuingia katika mashindano ya silaha na Marekani.
Hapo jana Msemaji wa Ikulu ya Russia (Kremlin), Dmitry Peskov alisema, Marekani inaituhumu Moscow kwamba imekiuka mkataba wa INF, lakini haijatoa nyaraka wala ushahidi wowote wa kuthibitisha tuhuma hizo, na kwamba uamuzi huo wa kujiondoa ulifikiwa kitambo sana.
Hii ni baada ya serikali ya Marekani kutangaza kusimamisha kwa muda utekelezaji wa mkataba wa Silaha za Nyuklia za Masafa ya Kati (INF).
Akitangaza uamuzi huo jana Ijumaa, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Mike Pompeo amesema yumkini Washington ikarejea katika mkataba huo katika muda wa siku 180, iwapo Russia itatekeleza matakwa ya Marekani, vingenevyo itajiondoa moja kwa moja.
Makubaliano hayo ya pande mbili ya kutokomeza Silaha za Nyuklia za Masafa ya Kati (INF) yalisainiwa mwaka 1987 na viongozi wa wakati huo wa Marekani na Shirikisho la Kisovieti la Urusi ya zamani na kutajwa kama hatua muhimu ya kuondoa hali ya mivutano katika enzi hizo za Vita Baridi.