OIC: Chuki na ubaguzi dhidi ya Waislamu vilifika kileleni mwaka jana
Kituo cha Islamophobia Watch kinachofuatilia chuki na ubaguzi unaofanyika dhidi ya Uislamu na Waislamu duniani kimetangaza kuwa, ubaguzi na chuki dhidi ya Waislamu vilifikia kileleni mwishoni mwa mwaka uliopita wa 2018.
Kituo hicho kinachofanya kazi chini ya Jumuiya ya Ushirikiano wa Nchi za Kiislamu (OIC) kimesema hayo katika ripoti yake ya 12 ya kila mwaka inayochunguza kipindi cha baina ya Juni mwaka 2018 hadi mwezi Februari mwaka huu.
Ripoti hiyo inasema kuwa, chuki na ubaguzi dhidi ya Waislamu vilishika kasi tena katika kipindi hicho baada ya kupungua kidogo. Imesisitiza kuwa ubaguzi na chuki dhidi ya Uislamu ilianza kama jibu lisilo la kimantiki la baadhi ya nchi kwa ajili ya kukabiliana na makundi yenye misimamo mikali na kueneza chuki hizo kwa jamii zote za Waislamu.

Ripoti hiyo ya OIC imesema kuwa, wimbi la chuki na ubaguzi dhidi ya Uislamu na Waislamu limepewa sura rasmi katika baadhi ya nchi na kuwa sehemu ya siasa za serikali za nchi husika kwa sababu ya uongozi wa wanasiasa na vyama vyenye misimamo mikali na ya kuchupa mipaka vya mrengo wa kulia ambavyo vinaupiga vita Uislamu.
Ripoti hiyo imezitaka nchi mbalimbali kufanya jitihada maradufu za kukabiliana na tatizo hilo kupitia sera za siasa za kitaifa na mitaala ya masomo mashuleni.