Mar 12, 2019 07:52 UTC
  • ICC: Waliohusika katika jinai dhidi ya Waislamu Warohingya kuchukuliwa hatua

Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) imesema watu waliohusika katika jinai za kutisha dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya nchini Myanmar watakabiliwa na mkono wa sheria na kubebeshwa dhima ya jinai hizo.

Baada ya kuzitembelea kambi za wakimbizi Warohingya nchini Bagladesh, Phakiso Mochochoko, Mkurugenzi wa Utawala wa ICC jana Jumatatu aliwaambia waandishi wa habari mjini Dhaka kuwa, licha ya kuwa Myanmar sio mwanachama wa Mkataba wa Roma uliounda mahakama hiyo, lakini hilo haliwezi kuwa kikwazo cha kuwawajibisha na kuwabebesha dhima wahusika wa jinai dhidi ya binadamu walizofanyiwa na wanazoendelea kufanyiwa Warohingya.

Septemba mwaka jana, Fatou Bensouda, Mwendesha Mashitaka Mkuu wa ICC alisema mahakama hiyo yenye makao yake mjini The Hague nchini Uholanzi imeanzisha uchunguzi wa awali wa kubaini iwapo kuna ushahidi wenye mashiko ambao utatoa waranti wa kuanzisha uchunguzi kamili kuhusu jinai za jeshi la Myanmar dhidi ya Waislamu wa Rohingya, yakiwemo mauaji, ubakaji na kufukuzwa makwao watu wa jamii hiyo ya wachache katika nchi hiyo ya kusini mashariki mwa bara Asia.

Mashirika ya kimataifa ya kutetea haki za binadamu yamekuwa yakishikilia kuwa, hatua za serikali ya Myanmar dhidi ya Waislamu wa Rohingya ni jinai za wazi dhidi ya binaadamu ambapo sambamba na kulaani jinai hizo yameitaka dunia kukabiliana na serikali ya nchi hiyo ili kuzuia hali hiyo.

Waislamu madhulumu wa Myanmar

Maelfu ya Waislamu wa kabila la Rohingya nchini Myanmar wameuawa na maelfu ya wengine kujeruhiwa tangu kuanza wimbi jipya la mashambulizi ya jeshi na Mabudha wenye misimamo mikali katika mkoa wa Rakhine magharibi mwa nchi nchi hiyo tangu tarehe 25 Agosti mwaka 2017 hadi sasa. 

Mauaji hayo ya umati dhidi ya Waislamu nchini Myanmar yamepelekea Waislamu wa Rohingya zaidi ya milioni moja kukimbilia hifadhi katika nchi jirani za Bangladesh na India.

 

Tags