Korea Kaskazini yaipa Marekani muhula na kuitaka ibadili mienendo
(last modified Sun, 14 Apr 2019 07:24:33 GMT )
Apr 14, 2019 07:24 UTC
  • Korea Kaskazini yaipa Marekani muhula na kuitaka ibadili mienendo

Kim Jong-un, Kiongozi wa Korea Kaskazini ameonya kuwa, mazungumzo mengine kati yake na Rais Donald Trump wa Marekani yatafanyika tu iwapo Washington itabadilisha mienendo na misimamo yake.

Shirika rasmi la habari la Korea Kaskazini KCNA jana Jumamosi lilimnukuu Kim Jong-un akiyasema hayo ambapo aliongeza kuwa, "Kinachotakiwa ni Marekani aingalie upya jinsi ya kupiga mahesabu na ije na mahesabu mapya."

Amesema atasubiri hadi mwishoni mwa mwaka huu kuona iwapo Marekani itachukua uamuzi. Kiongozi wa Korea Kaskazini amebainisha kuwa, Marekani iko katika hatari ya kurejea kwenye taharuki iliyokuwa nayo huku nyuma, baada ya mkutano wa pili kati yake na Trump kugonga mwamba.

Mkutano wa pili kati ya Trump na Kim Jong-un wa Korea Kaskazini ulifanyika kati ya tarehe 27 na 28 ya Februari mwaka huu mjini Hanoi, Vietnam ambapo ulimazika bila kufikiwa natija yoyote.

Kim na Trump

Viongozi wa Korea Kaskazini walitangaza kwamba hatua ya kupenda makubwa ya rais huyo wa Marekani ndio iliyopelekea mazungumzo hayo kuvunjika. Duru ya kwanza ya mazungumzo ya viongozi hao ilifanyika tarehe 12 Juni mwaka jana nchini Singapore. 

Hii ni katika hali ambayo, Rais Moon Jae-in wa Korea Kusini ametaka kuendelezwa mazungumzo kati ya Marekani na Korea Kaskazini kwa ajili ya kutatua mzozo wa eneo la Rasi ya Korea.

Tags