Umoja wa Mataifa watoa pongezi za Ramadhani
(last modified Mon, 06 May 2019 03:50:34 GMT )
May 06, 2019 03:50 UTC
  • Umoja wa Mataifa watoa pongezi za Ramadhani

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametoa mkono wa pongezi na fanaka kwa Waislamu wote duniani kwa mnasaba wa mwezi mtukufu wa Ramadhani

Kwa mujibu wa shirika la habari la IRNA, António Guterres ameandika katika ukurasa wake wa Twitter kwa lugha mbili za Kiarabu na Kiingereza kwamba anawatakia Waislamu wote mwezi mwema uliojaa fadhila wa Ramadhani ambao ni chemchemu ya ilhamu njema kwa dunia nzima.

Baadhi ya nchi duniani kama vile Saudia, Kuwait, Bahrain, Umoja wa Falme za Kiarabu n.k, zimeanza leo kufunga mwezi mtukufu wa Ramadhani baada ya kukamilisha siku 30 za Shaabani kwa mujibu wa kalenda zao.

António Guterres

 

Nchi nyingine kama hapa Iran, Tanzania, Oman, Iraq, China, Australia, New Zealand, Pakistan na nyinginezo nyingi, leo zinakamilisha mwezi 30 Shaaban na kesho tukijaaliwa ndio siku ya kwanza ya mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Mwezi mtukufu wa Ramadhani ni mwezi wenye fadhila nyingi, ni mwezi ambao ndani yake imeshushwa Qur'ani Tukufu, ni mwezi ambao Bwana Mtume Muhammad SAW ameuita ni wa Mwenyezi Mungu. Katika mwezi wa Ramadhani kila kitu cha Muislamu mwenye kufunga huwa kinaandikiwa thawabu hata kulala kwake. Ni mwezi ambao mapenzi na udugu baina ya Waislamu huongezeka mno ikilinganishwa na miezi mingine ya mwaka.

Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran inawaombea Waislamu wote kheri za mwezi huo mtukufu ambao ni hiba, atia na zawadi kubwa sana itokayo kwa Mwenyezi Mungu kwa ajili ya waja Wake anaowapenda.