Venezuela yaweka kando matumizi ya sarafu ya dola
(last modified Fri, 10 May 2019 03:57:39 GMT )
May 10, 2019 03:57 UTC
  • Venezuela yaweka kando matumizi ya sarafu ya dola

Rais wa Venezuela ametangaza kuwa nchi hiyo inaweka kando matumizi ya sarafu ya dola ya Marekani kwa sababu haitaki kutegemea mfumo wa fedha wa nchi ajinabi.

Rais Nicolas Maduro amesisitiza kuwa Venezuela inaweza kutekeleza shughuli zake za kiuchumi bila ya kutegemea sarafu ya dola au mfumo wa fedha wa nchi ajinabi. Rais wa Venezuela amesema kuwa kuna ulazima wa kufanyika mabadiliko makubwa ili kukabiliana na mzingiro wa Marekani. Benki Kuu ya Venezuela pia tayari imechapisha hati ambayo kwa mujibu wake siasa za soko huru la fedha za kigeni nchini humo zimesitishwa.  

Kabla ya kuchukuliwa hatua hii, ununuaji na uuzaji wa fedha zote za kigeni ikiwemo dola ulikuwa huru katika benki za biashara za Venezuela. Serikali ya nchi hiyo siku zote imekuwa ikizingatia udhibiti wa soko la fedha hizo za kigeni. Hali ya mgogoro imepamba moto hivi sasa nchini Venezuela tangu Juan Guaido kiongozi wa wapinzani wa serikali ya Maduro alipojitangaza mwishoni mwa mwezi Januari mwaka huu kuwa Rais wa muda wa nchi hiyo huku akiungwa mkono na Marekani na baadhi ya nchi za eneo. Russia, Iran Bolivia, China, Cuba na baadhi ya nchi nyingine duniani zimetangaza kumuunga mkono Rais halali wa Venezuela Nicolaus Maduro.   

Juan Guaido, kiongozi wa upinzani Venezuela anayeungwa mkono pakubwa na Marekani 

 

Tags