Jeshi la Venezuela lasema liko tayari kukabiliana na Marekani
(last modified Sun, 19 May 2019 07:55:23 GMT )
May 19, 2019 07:55 UTC
  • Jeshi la Venezuela lasema liko tayari kukabiliana na Marekani

Jeshi la Venezuela limetangaza utiifu kamili kwa serikali ya Rais Nicholas Maduro wa nchi hiyo na kusema liko na silaha mkononi tayari kukabiliana na hujuma yoyote ya kijeshi dhidi ya nchi hiyo.

Wanajeshi wa Venezuela wametoa taarifa Jumamosi baada ya kushiriki katika 'Gwaride la Utiifu'  ambapo wametangaza utiifu wao kwa Rais Maduro.

Wanajeshi hao wamesema katu hawatairuhusu Marekani imefanikiwe katika hujuma dhidi ya nchi hiyo. Rais Maduro alitembea umbali wa maili moja akiwa pamoja na wanajeshi hao kabla ya kutoa hotuba kali ya kulaani ubeberu na ukoloni mamboleo wa Marekani.

Ikumbukwe kuwa, baada ya kushindwa katika uchaguzi wa rais, kinara wa upinzani Venezuela Juan Guaido alijitangaza kuwa rais wa muda hapo tarehe 23 Januari mwaka huu kupitia uungaji mkono kamili wa Marekani.

Kinara wa upinzani Venezuela Juan Guaido (kulia) anapata uungaji mkono kamili wa Rais Trump wa Marekani

Hata hivyo licha ya njama hizo za kutaka kumuondoa madarakani Rais Maduro, jeshi na wananchi pamoja na nchi kama vile Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Russia, China, Afrika Kusini na mataifa mengi ya dunia yameendelea kusisitizia ulazima wa kuheshimiwa haki ya kujitawala nchi hiyo ya Amerika ya Latini.

 

Tags