Nchi za Ulaya zinaziuzia nchi za Afrika dizeli inayoua
https://parstoday.ir/sw/news/world-i53942-nchi_za_ulaya_zinaziuzia_nchi_za_afrika_dizeli_inayoua
Mtaalamu maalum wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa kuhusu taka hatarishi na za sumu amezionya kampuni za Ulaya ambazo zinaziuzia nchi za Afrika nishati chafuzi yakiwemo mafuta ya dizeli yenye kemikali za sumu.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jun 06, 2019 02:33 UTC
  • Nchi za Ulaya zinaziuzia nchi za Afrika dizeli inayoua

Mtaalamu maalum wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa kuhusu taka hatarishi na za sumu amezionya kampuni za Ulaya ambazo zinaziuzia nchi za Afrika nishati chafuzi yakiwemo mafuta ya dizeli yenye kemikali za sumu.

Katika taarifa iliyotolewa kwa mnasaba wa Siku ya Mazingira Duniani iliyoadhimishwa Juni 5, Mtaalamu huyo Baskut Tuncak amesema ni ajabu kuona kampuni hizo kutoka Ulaya zikiziuzia nchi za Afrika dizeli ambayo katu haiwezi kuuzwa kwenye masoko ya Ulaya, akisema tabia hiyo ikome kwa kuwa inasababisha uchafuzi wa  hewa na vifo.

Kupitia taarifa iliyotolewa mjini Geneva, Uswisi na Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa, mtaalamu huyo amesema biashara hiyo ambayo ni kinyume na maadili na sheria, husababisha uchafuzi wa hewa ambayo ndio maudhui ya siku ya mazingira duniani mwaka huu.

Amesema dizeli hiyo chafu inakadiriwa kuua maelfu ya watu barani Afrika kila mwaka na idadi hiyo ya vifo inaweza kufikia 31,000 ifikapo mwaka 2030 iwapo suala hilo halitashughulikiwa.

Uchafuzi wa mazingira katika mji wa Kampala nchini Uganda

Tuncak amesema kitendo cha kujinufaisha na viwango vidogo vilivyowekwa na Afrika ni kinyume na maadili lakini pia ni uhalifu ambao lazima uachwe na kwamba Afrika na Ulaya lazima zisake njia bora na ya wazi ya kuwa na nishati isiyo na kemikali za sumu na iliyo salama.

Kwa mujibu wa sheria ya kimataifa, ni uhalifu kuiuzia nchi nyingine mada zenye sumu ikiwemo nishati ambayo imepigwa marufuku kwenye nchi nyingine ambayo ni mwanachama wa Mkataba wa Kimataifa wa Bamako hata kama nchi inayouza bidhaa hiyo si mwanachama wa mkataba huo.

Mataifa 27 ya Afrika yameridhia mkataba wa Bamako na mtaalamu huyo ametaka serikali za Ulaya na Afrika zihakikishe kuwa kampuni za biashara zinaheshimu haki za binadamu za kila mtu ikiwemo ya kuvuta  hewa safi.