Kuendelea juhudi za utatuzi wa mgogoro wa Venezuela
(last modified Sun, 16 Jun 2019 10:29:14 GMT )
Jun 16, 2019 10:29 UTC
  • Kuendelea juhudi za utatuzi wa mgogoro wa Venezuela

Baada ya wapinzani wa Rais Nicolás Maduro wa Venezuela kufeli katika njama zao na kisha nchi hiyo kukumbwa na mkwamo wa kisiasa, kumeanza juhudi za kimataifa za kuondoa mkwamo huo.

Hii ni kusema kuwa, Stéphane Dujarric, Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameelezea maendeleo ya juhudi za kutatuliwa mzozo wa nchi hiyo ya Amerika ya Latini na kuongeza kwamba: "Kikao cha wawakilishi wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya mzozo wa Venezuela kimefanyika kwa mara ya kwanza na kuishirikisha pia serikali ya Sweden katika kikao cha faragha." Washiriki wa mkutano huo sambamba na kutangaza uungaji mkono wao kwa mwenendo wa amani na utulivu nchini Venezuela, walijadili pia mwenendo wa mazungumzo ya Norway sanjari na kuunga mkono njia ya utatuzi wa amani kwa ajili ya kuimarisha usalama nchini Venezuela. Kadhalika Michelle Bachelet, Kamishna Mkuu wa Haki za Binaadamu wa Umoja wa Mataifa na katika safari yake nchini Venezuela alikutana kwa nyakati tofauti na Rais Nicolás Maduro na Juan Guaidó, kiongozi wa upinzani wa nchi hiyo. Mgogoro wa Venezuela hata kama umekuwepo kwa muda mrefu sasa, lakini ulishtadi kuanzia tarehe 23 Januari mwaka huu, baada ya Juan Guaidó, kiongozi wa upinzani kujitangaza kuwa rais wa muda wa nchi hiyo ya Amerika ya Latini ambapo uliingia katika hatua mpya.

Jeshi la Venezuela lililojiweka tayari kukabiliana na njama chafu za Marekani

Ni miezi sita imepita tangu wapinzani wa ndani dhidi ya Rais Nicolás Maduro na wanaopata uungaji mkono wa Marekani, wamekuwa wakitekeleza hatua haribifu na zisizo za kisheria nchini humo. Marekani na katika uungaji mkono wake kwa wapinzani hao, ilishadidisha mashinikizo ya kiuchumi, kisiasa na kiusalama dhidi ya serikali halali ya Rais Maduro. Kuweka vikwazo vikali katika sekta ya nishati, sekta za kifedha na kibenki za nchi hiyo, kuwaunga mkono wafanya mapainduzi ya kijeshi na kutoa vitisho vya kijeshi, ni miongoni mwa hatua za Washington dhidi ya serikali ya Caracas ambazo hata hivyo zimeishia kugonga mwamba. Licha ya mashinikizo yote ya Marekani, lakini Rais Nicolás Maduro na chini ya uungaji mkono wa wananchi na jeshi la Venezuela, ameweza kuyashinda matatizo na kuendelea kusalia madarakani kama rais halali wa nchi hiyo. Katika upande mwingine, Diosdado Cabello, Spika la Baraza la Waasisi nchini Venezuela sambamba na kuashiria kwamba njama za Marekani za kuzusha ghasia nchini humo zimefeli na badala yake kuishia kuibuka tofauti katika safu ya wapinzani, amesema: "Serikali ya Venezuela iko tayari kufanya mazungumzo na nchi yoyote ile." Tangu mwezi mmoja uliopita, baadhi ya nchi kwa kushirikiana na asasi za kimataifa, zimekuwa zikifanya juhudi za kurejesha usalama na utulivu nchini Venezuela pamoja na kuhitimisha mzozo huo. Moja ya nchi hizo ni Norway ambayo ilitangaza kuwa iko tayari kuwa mpatanishi. Tayari Norway imeshasimamia mazungumzo ya amani ya duru mbili kati ya serikali na wapinzani. Pamoja na kwamba wengi walitaraji kuwa mwenendo wa mazungumzo hayo ungesaidia kuinasua Venezuela kutoka katika mkwamo huo wa kisiasa, lakini mazungumzo hayo pia yamekwamishwa na wapinzani ambao wanaungwa mkono na Marekani kwa nguvu zote.

Sisitiza la Wavenezuela la kuitaka Marekani iache kufuatilia mambo ya ndani ya nchi yao

Wapinzani hao ambao walitaka kuondoka madarakani Rais Maduro, kuundwa serikali ya mpito na kisha kuitishwa uchaguzi wa mapema wa urais, baada ya duru ya pili ya kikao cha Oslo, mji mkuu wa Norway awali waliamua kususia mazungumzo hayo. Hata hivyo wapinzani hao hivi sasa wamekubali kubakia kwenye mazungumzo. Sababu ya jambo hilo la mara kukataa na mara kukubali, inaonekana kwamba ni kitendo cha serikali ya Marekani cha kuendeleza siasa zake hasi za mashinikizo na vitisho dhidi ya Venezuela na kuzuka tofauti katika safu ya wapinzani wa serikali, ndiko kulikowafanya wapinzani hao kukubali kuendelea na mazungumzo. Mike Pompeo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani ameashiria tofauti zilizojitokea kati ya wapinzani wa serikali na kusema kuwa tofauti hizo zinaweza kumalizika kwa maslahi ya Rais Nicolás Maduro. Amesema: "Kulinda umoja wa wapinzani limekuwa ni jambo gumu hivi sasa." Udhaifu wa Juan Guaidó uliomfanya ashindwe kuwaongoza wapinzani kutokana na kujiegemeza kwa Marekani katika kila kitu, na wakati huo huo kuendelea uungaji mkono wa wananchi kwa Rais Maduro, ni mambo yaliyopelekea mrengo wa upinzani wa ndani nchini Venezuela kudhoofika sana. Ni kwa ajili hiyo ndio maana inaonekana kuwa, kuendelea mazungumzo na serikali kwa ajili ya kuodokana na hali mbaya ya sasa ni moja ya machaguo yanayotakiwa na wapinzani hao wa serikali ya Venezuela.

Tags