Jul 05, 2019 07:13 UTC
  • Mwendesha Mashtaka wa ICC ataka kuchunguzwa jinai dhidi ya Warohingya

Mwendesha Mashitaka wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) ametoa mwito wa kuanzishwa uchunguzi wa jinai za kutisha dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya nchini Myanmar, akisisitiza kuwa wahusika wanapaswa kukabiliwa na mkono wa sheria na kubebeshwa dhima ya jinai hizo.

Kwa mujibu wa nyaraka za mahakama hiyo, Mwendesha Mashtaka huyo wa ICC ambaye jina lake halijatajwa amesema kuna ushahidi wenye mashiko unaoonyesha kuwa wanajeshi, polisi na raia wa Myanmar walitenda jinai za kutisha dhidi ya Warohingya. 

Ombi hilo la Mwendesha Mashitaka wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai limekuja siku chache baada ya timu ya uchunguzi ya Umoja wa Mataifa kuonya kuwa, visa vipya vya jinai na kukanyagwa haki za binadamu vinafanywa na maafisa usalama wa Myanmar dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya.

Septemba mwaka jana, Fatou Bensouda, Mwendesha Mashitaka Mkuu wa ICC alisema mahakama hiyo yenye makao yake mjini The Hague nchini Uholanzi imeanzisha uchunguzi wa awali wa kubaini iwapo kuna ushahidi wenye mashiko ambao utatoa waranti wa kuanzisha uchunguzi kamili kuhusu jinai za jeshi la Myanmar dhidi ya Waislamu wa Rohingya, yakiwemo mauaji, ubakaji na kufukuzwa makwao watu wa jamii hiyo ya wachache katika nchi hiyo ya kusini mashariki mwa bara Asia.

Wanajeshi wa Myanmar wanashirikiana na Mabudha kuwakandamiza Waislamu wa Rohingya

Mashirika ya kimataifa ya kutetea haki za binadamu yanasisitiza kuwa, hatua za serikali ya Myanmar dhidi ya Waislamu wa Rohingya ni jinai za wazi dhidi ya binadamu ambapo sambamba na kulaani jinai hizo yameitaka dunia kukabiliana na serikali ya nchi hiyo ili kuzuia hali hiyo.

Maelfu ya Waislamu wa kabila la Rohingya nchini Myanmar wameuawa na maelfu ya wengine kujeruhiwa tangu kuanza wimbi jipya la mashambulizi ya jeshi na Mabudha wenye misimamo mikali katika mkoa wa Rakhine magharibi mwa nchi nchi hiyo tangu tarehe 25 Agosti mwaka 2017, ambapo mbali na mauaji hayo,  wengine zaidi ya milioni moja wamelazimika kukimbilia hifadhi katika nchi jirani za Bangladesh na India.

Tags