Umoja wa Ulaya warefusha vikwazo kwa Korea ya Kaskazini
(last modified Wed, 17 Jul 2019 02:35:17 GMT )
Jul 17, 2019 02:35 UTC
  • Umoja wa Ulaya warefusha vikwazo kwa Korea ya Kaskazini

Baraza la Umoja wa Ulaya limerefusha muda wa vikwazo vyake dhidi ya Korea ya Kaskazini ikiwa ni radiamali yake kwa majaribio ya makombora na silaha za nyuklia ya nchi hiyo.

Baraza la Masuala ya Nje la Umoja wa Ulaya limetoa taarifa likijibu shuguli za nyuklia na makombora zinazofanywa na Korea ya Kaskazini na kwa mara nyingine tena kuwawekea vikwazo shakhsiya 57 na taasisi 9 za nchi hiyo. Vikwazo hivyo vinajumuisha marufuku ya kusafiri nje ya nchi na kuzuiwa mali za watu na taasisi zilizoorodheshwa kwenye orodha ya vikwazo vya Umoja wa Ulaya.  

Umoja wa Ulaya uliiwekea vikwazo Korea ya Kaskazini kwa mara ya kwanza mwaka 2006. Sambamba na kurefusha vikwazo hivyo imeelezwa kuwa timu za wataalamu kutoka Washington na Pyongyang zinajiandaa kuanza mazungumzo kujadili miradi ya nyuklia ya Korea ya Kaskazini. Marekani pia imeiwekea Korea ya Kaskazini vikwazo vya upande mmoja kutokana  na miradi yake ya nyuklia na makombora na hivi sasa serikali ya Trump inafanya kila iwezalo kuilazimisha Pyongyang iachane na miradi yake ya nyuklia. 

Rais wa Marekani na Kiongozi wa Korea ya Kaskazini wameshakutana mara tatu huko Singapore, Vietnam na katika eneo lisilo la kijeshi lililopo kati ya Korea mbili; hata hivyo  vikao hivyo vimeshindwa kuzaa matunda. 

Kiongozi wa Korea ya kaskazini na Rais wa Marekani walipokutana huko Singapore  
 

 

Tags