Umoja wa Ulaya wamwonya Boris Johnson kuhusiana na Brexit
https://parstoday.ir/sw/news/world-i54981-umoja_wa_ulaya_wamwonya_boris_johnson_kuhusiana_na_brexit
Hatimaye baada ya kusubiriwa kwa muda mrefu, uamuzi wa kumchagua kiongozi wa chama cha Wahafidhina na Waziri Mkuu wa Uingereza umechukuliwa, baada ya Boris Johnson kuchaguliwa kuhudumu katika nafasi hizo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 25, 2019 06:18 UTC
  • Umoja wa Ulaya wamwonya Boris Johnson kuhusiana na Brexit

Hatimaye baada ya kusubiriwa kwa muda mrefu, uamuzi wa kumchagua kiongozi wa chama cha Wahafidhina na Waziri Mkuu wa Uingereza umechukuliwa, baada ya Boris Johnson kuchaguliwa kuhudumu katika nafasi hizo.

Kuchaguliwa kiongozi huyo kumezua wimbi kubwa la hofu na wasiwasi katika Umoja wa Ulaya kutokana na misimamo yake mikali kuhusiana na suala zima la Uingereza kujiondoa katika umoja huo, mashuhuri kama Brexit. Huku ukimpongeza kwa kuchaguliwa kuwa Waziri Mkuu mpya wa Uingereza, Umoja wa Ulaya hata hivyo umemwonya mapema kwamba hakutakuwepo na mabadiliko yoyote katika mazungumzo ya kujitoa nchi hiyo katika umoja huo. Umemwonya kwamba atakuwa na kipindi kigumu siku zijazo na kwamba ahadi yake ya kufanyika uchaguzi kwa ajili ya kufanya mazungumzo mapya na umoja huo haitatekelezwa. Licha ya viongozi wa ngazi za juu wa Umoja wa Ulaya kumpongeza Boris Johnson kwa kuteuliwa kuwa Waziri Mkuu mpya wa Uingereza lakini dalili zilizopo zinaonyesha wazi kwamba hawako tayari kufanya mazungumzo mapya na Uingereza kuhusiana na uamuazi wa nchi hiyo kujiondoa katika umoja huo.

Huku akielezea matunaini ya kuwepo uhusiano mzuri kati ya London na Brussels, Ursula von der Leyen, Mkuu mpya wa Kamisheni ya Umoja wa Ulaya amesema: Tutakuwa na changamoto nyingi katika siku zijazo.

Hivi sasa Johnson ana muda wa miezi mitatu pekee yaani kufikia tarehe 31 Oktoba awe ameiondoa Uingereza katika Umoja wa Ulaya. Katika siku za kampeni za uchaguzi, aliahidi kuitoa Uingereza katika Umoja wa Ulaya ima kwa kufikiwa mapatano au bila ya kufikiwa mapatano na umoja huo.

Ursula von der Leyen, Mkuu mpya wa Kamisheni ya Umoja wa Ulaya

Suala la Brexit limeendelea kuibua changamoto za kisiasa, kiuchumi na kiusalama ambapo wajuzi wa amambo wanaamini kwamba kujitoa Uingereza katika Umoja wa Ulaya bila kufikiwa mapatano na umoja huo huenda kukaisababishia matatizo makubwa ya kiuchumi. Moja ya matokeo ya moja kwa moja ya kujitoa Uingereza katika Umoja wa Ulaya ni kuwekewa ushuru wa forodha bidhaa za nchi hiyo zinazoingizwa katika nchi wanachama wa umoja huo. Uzalishaji bidhaa za ndani wa nchi hiyo pia unatazamiwa kupungua kwa asilimia 2 kufikia mwaka 2020.

Kinyume na alivyokuwa akiamini Theresa May, Waziri Mkuu wa Uingereza aliyejiuzulu hivi karibuni, aliyesema kuwa nchi hiyo haipasi kujitoa katika Umoja wa Ulaya bila kufikiwa mapatano na Brussels, makao makuu ya Umoja wa Ulaya, Boris Johnson anaamini kwamba nchi hiyo inapasa kujitoa katika umoja huo kwa hali yoyote ile hata bila ya kufikiwa mapatano na umoja huo. Ni wazi kuwa kama Johnson atatekeleza ahadi yake hiyo basi Uingereza itakabiliwa na changamoto kubwa. Katika hatua ya kwanza changamoto hizo zitaanza kuonekana ndani ya Uingereza yenyewe, jambo linaloweza kuhatarisha nafasi yake ya kisiasa ndani ya nchi na chama chake mwenyewe. Hii ni kwa kuwa wananchi wa Uingereza hawako tayari kushuhudia matatizo ya kujitoa nchi hiyo katika Umoja wa Ulaya yakiwadhuru moja kwa moja.

Theresa May, Waziri Mkuu wa Uingereza aliyejiuzulu

Kwa sasa viongozi wengi wa Uingereza wana wasiwasi mkubwa kuhusiana na uendeshaji mambo ya nchi hiyo katika kipindi cha uongozi wa Boris Johnson. Wakati huohuo viongozi wa Umoja wa Ulaya tayari wametangaza kuwa hawatakubali kufanyika mabadiliko yoyote katika mazungumzo yanayohusiana na kujiondoa nchi hiyo katika umoja huo. Hata hivyo licha ya viongozi hao kuchukua msimamo huo lakini baadhi ya dalili zinaonyesha kuwa wako tayari kuongeza muda wa kujiondoa Uingreza katika umoja huo.

Kuhusiana na hilo, Ursula von der Leyen, Mkuu wa Kamisheni ya Ulaya amesema kuwa kuna uwezekano wa kuongezwa muda wa Brexit iwapo Boris Johnson atawasilisha sababu mpya za kutaka muda huo uongezwe.

Pamoja na hayo inaonekana kuwa Johnson hana nia yoyote ya kutaka kuongezewa muda huo na ameazimia kuiburuta Uingereza nje ya umoja huo kufikia Oktoba 31, hata kwa thamani ya kuhatarisha nafasi yake ya kisiasa nchini humo.