Russia yaituhumu Marekani na nchi za Ulaya kuwa zimechochea machafuko Moscow
Msemaji wa Wizara ya Mambo y Nje ya Russia amesema kuwa Marekani na baadhi ya nchi za Ulaya zimehusika katika machafuko yaliyotokea hivi karibuni mjini Moscow.
Maria Zakharova amekosoa uingiliaji kati wa Marekani na nchi kadhaa za Ulaya katika mambo ya ndani ya Russia na kusema kuwa: Nchi hizo zilikuwa na nia ya kupanua machafuko hayo katika miji mingine ya Russia.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia ameongeza kuwa, katika siku za hivi karibuni balozi za Marekani na nchi kadhaa za Ulaya mjini Moscow zikishirikiana na vyombo vyao vya habari zilifanya jitihada za kuchochea machafuko katika maandamano halali yaliyofanyika Moscow.
Zakharova amesisitiza kuwa, Jumamosi iliyopita ubalozi wa Marekani mjini Moscow ulisambamba matangazo yanayoainisha njia ya maandmano dhidi ya serikali katika jiji hilo na kuwahimiza wananchi kushiriki katika maandamano hayo.
Amesema kuwa zinachukuliwa hatua za kidiplomasia za kuitaka Marekani na nchi za Ulaya zikome kuingilia masuala ya ndani ya Russia.
Katika maandamano na ghasia za siku kadhaa zilizopita mjini Moscow watu zaidi ya 600 walitiwa nguvuni na kukabidhiwa kwa vyombo vya mahakama kwa tuhuma za kuzusha machafuko na kuvuruga amani na nidhamu.