Aug 07, 2019 07:06 UTC
  • UN yatilia mkazo udharura wa kujiepusha na matamshi yanayochochea chuki duniani

Msemaji wa Kamisheni Kuu ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa amekemea mauaji ya ufatuaji risasi wa hivi karibuni nchini Marekani na kuwataka viongozi wa nchi mbalimbali kujiepusha kutoa matamshi yanayochochea chuki dhidi ya jamii za waliowachache.

Rupert Colville amesema Umoja wa Mataifa unalaani ubaguzi wa rangi, hisi za kuwapiga vita wageni na chuki na taasubi za aina zote ikiwa ni pamoja na kuwatambua watu weupe kuwa ndio bora zaidi na unawataka viongozi wa nchi mbalimbali ikiwemo Marekani, kuchukua hatua chanya za kukomesha kabisa ubaguzi na utumiaji wa mabavu.

Kuhusu matamshi yanayotolewa na Rais Donald Trump wa Marekani dhidi ya wahajiri ambayo yanachochea ubaguzi wa rangi, Colville amesisitiza kuwa, Umoja wa Mataifa una wasiwasi kwamba matamshi kama haya mbali ya kutoa ujumbe unaowachafulia jina wahajiri, wakimbizi na wanawake na kuwashushia hadhi yao kama wanadamu, yanachochea mashambulizi na vitendo vya kulipiza kisasi.

Tarehe 3 na 4 mwezi huu wa Agosti Marekani ilikuwa uwanja wa mashambulizi ya ufyatuaji risasi uliochochewa na ubaguzi wa rangi katika miji ya El Paso jimboni Texas, Dayton huko Ohio na Chicago katika jimbo la Illinois. Mashambulizi hayo yamesababisha vifo vya makumi ya watu na kujeruhi wengine wengi.

Tags