EU yasisitiza kupatiwa ufumbuzi mzozo wa Kashmir kwa njia ya kisiasa
Umoja wa Ulaya (EU) umetangaza kuwa utatuzi wa kisiasa ndio njia pekee inayoweza kumalizika hitilafu katika eneo la Kashmir kati ya India na Pakistan.
Msemaji wa Masuala ya Nje na Usalama wa Umoja wa Ulaya Maja Kocijancic amesema kuwa umoja huo unaunga mkono suala la kupatika njia ya kisiasa ya kutatua hitilafu baina ya pande mbili za India na Pakistan kuhusu ya eneo la Kashmir ambazo zimeuibua hali ya machafuko na ukosefu wa amani katika eneo hilo.
Kocijancic ameongeza kuwa, Umoja wa Ulaya unafanya kila uwezalo katika uga wa diplomasia ili kuzipatia ufumbuzi hitilafu zilizojitokeza kuhusiana na eneo la Kashmir.
Serikali ya India tarehe 5 mwezi huu ilitangaza kuwa imechukua uamuzi wa kulifutia mamlala mahsusi ya kujitawala eneo la Kashmir, hatua iliyokosolewa na kupingwa vikali na Wakshmir na serikali ya Pakistan.
Pakistan pia imetahadharisha kuhusu mpango wa India wa kufuta kizazi cha Waislamu wa eneo la Jammu na Kashmir na kueleza kuwa, New Delhi ina lengo la kulivamia kijeshi eneo la Kashmir linalodhibitiwa na Pakistan.
Itafahamika kuwa, sehemu moja ya Kashmir iko chini ya udhibiti wa India na nyingine iko Pakistan. Nchi zote mbili zinadai kuwa wamiliki wa eneo lote la Kashmir yote. Suala hili ni moja ya sababu kuu zilizoibua tena mzozo huu wa siku nyingi kati ya New Delhi na Islamabad ulioanza tangu Pakistan ijitenge na India mwaka 1947.