Uafriti wa Marekani wa kukwamisha mazungumzo ya Rasi ya Korea
(last modified Thu, 03 Oct 2019 04:13:59 GMT )
Oct 03, 2019 04:13 UTC
  • Uafriti wa Marekani wa kukwamisha mazungumzo ya Rasi ya Korea

Mwakilishi wa Korea Kaskazini katika Umoja wa Mataifa amesema, kuhalifu Marekani ahadi zake ndiko kulikosababisha kusita mazungumzo ya nyuklia kati ya nchi mbili. Akihutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Kim Song amebainisha kuwa: Hali ya mambo katika Rasi ya Korea ingali inazidi kutokota joto la mivutano, suala ambalo limetokana na hatua za kichochezi za kijeshi na kisiasa za Marekani.

Kim Song, Mwakilishi wa Korea Kaskazini UN

Matamshi hayo ya mwakilishi wa Korea Kaskazini katika Umoja wa Mataifa yametolewa katika hali ambayo tangu Juni mwaka uliopita wa 2018 hadi sasa, kiongozi wa nchi hiyo Kim Jong Un na Rais Donald Trump wa Marekani wamekutana na kufanya mazungumzo mara tatu huko Singapore, Vietnam na katika mpaka wa pamoja wa Korea mbili za Kaskazini na Kusini, lakini mazungumzo hayo ya pande mbili bado hayajazaa matunda na hivi sasa yamesitishwa. Kwa muktadha huo, suali la kujiuliza hapa ni, kwa nini licha ya kufanyika vikao vitatu, tena katika ngazi ya viongozi wa juu kabisa wa serikali za Marekani na Korea Kaskazini, ukuta wa hali ya kutoaminiana ungali bado ni mrefu kati ya Pyongyang na Washington; na licha ya kupita zaidi ya mwaka mmoja sasa hatua iliyofikiwa katika mazungumzo baina ya pande mbili ingali si ya kuridhisha hata kidogo?

Trump (kulia) na Kim walipokutana kwa mara ya kwanza nchini Singapore

Aghalabu ya wataalamu wa siasa wanaitakidi kuwa, hali ya kutoaminiana inayotawala katika uhusiano wa Marekani na Korea Kaskazini inatokana na sababu za kadhaa za msingi. Ya kwanza ni kwamba, Korea Kaskazini inataka ipunguziwe vikwazo ilivyowekewa na Marekani, lakini Washington inasisitiza kwamba ni Pyongyang inayopaswa kwanza kuchukua hatua kadhaa katika kutokomeza silaha zake za nyuklia kabla ya kupunguzwa vikwazo ilivyowekewa. Zaidi ya hayo ni kwamba, kwa mtazamo wa Korea Kaskazini, licha ya hatua kadhaa za dhati ilizochukua kwa ajili ya kujenga hali ya kuaminiana na kutekeleza taarifa ya pamoja ya kikao cha kwanza cha pamoja cha Kim na Trump kilichofanyika Singapore, Marekani haijachukua yoyote ya kutekeleza taarifa hiyo ya pamoja; na badala yake, mazoezi ya kijeshi kati ya nchi hiyo na Korea Kusini, ambayo Trump aliahidi kuwa yatasisimamishwa yameanza tena, na vikwazo dhidi ya Pyongyang vimeshadidishwa. Inavyoamini Korea Kaskazini, kufanyika manuva ya pamoja baina ya Marekani na Korea Kusini, ni tishio kwa nchi hiyo, hatua ambayo lengo lake hasa ni kuiangusha serikali ya Pyongyang. Kwa mtazamo wa Korea Kaskazini, kufanyika mazoezi ya aina hiyo ya kijeshi kunakiuka makubaliano na mazungumzo ya pande mbili na ni mkakati wa maandalizi kwa ajili ya kuishambulia kijeshi nchi hiyo.

Mazoezi ya pamoja ya kijeshi ya Marekani na Korea Kusini

Hata hivyo la ajabu zaidi ni kwamba, katika hali na mazingira kama hayo, Trump amesikika hivi karibuni akisema kuwa, ana hamu ya kukutana na kiongozi wa Korea Kaskazini kwa ajili ya kikao kingine cha nne. Hata hivyo maafisa wa Pyongyang wamesisitiza kuwa, ikiwa Marekani haitatoa pendekezo la kuweza kukubalika, hawatorudi kwenye meza ya mazungumzo. Aidha wamesema wana matumaini kwamba, ili Rais wa Marekani aweze kukutana  na kuketi tena pamoja na kiongozi wa Korea Kaskazini kwenye meza ya mazungumzo, inabidi afanye chagua la kimantiki na kuchukua uamuzi wenye uwazi.

Kwa ujumla ni kwamba, wakati viongozi wa Pyongyang wanaibebesha Marekani dhima ya kukwama mazungumzo ya nyuklia kati ya nchi mbili, kwa mtazamo wa aghalabu ya wadadisi wa masuala ya kisiasa, pamoja na kupita zaidi ya mwaka mmoja tangu vilipofanyika vikao vitatu kati ya Kim na Trump, kuendelezwa mbinu ya mashinikizo na kushadidishwa vikwazo vya Marekani dhidi ya Korea Kaskazini, mbali na Marekani na Korea Kusini kutotekeleza ahadi zao, hasa kwa kufanya mazoezi kadhaa ya pamoja ya kijeshi, ndiyo sababu ya kushindwa kuendelea mazungumzo ya nyuklia katika Peninsula ya Korea. Kwa kuyaelewa yote hayo, viongozi wa Pyongyang wanasisitiza kuwa, ni juu ya Marekani kuamua kama mazungumzo ni fursa au ni njia ya kushadidisha mgogoro katika eneo hilo.../

Tags