Apr 30, 2024 07:21 UTC
  • UN: Kombora la balestiki la Korea Kaskazini limetumika kushambulia mji wa Kharkiv, Ukraine

Wachunguzi wa vikwazo wa Umoja wa Mataifa wameiambia kamati ya vikwazo ya Baraza la Usalama la umoja huo kuwa, mabaki ya kombora yaliyopatikana katika mji wa Kharkiv nchini Ukraine mnamo Januari 2 yanatokana na kombora la balestiki la Korea Kaskazini aina ya Hwasong-11.

Katika ripoti yao ya kurasa 32, wachunguzi hao wa vikwazo wa Umoja wa Mataifa wamefikia hitimisho kwamba, mabaki yaliyopatikana kwenye kombora lililotua Kharkiv, Ukraine, mnamo Januari 2, 2024 yametokana na kombora la Korea Kaskazini aina ya Hwasong-11 na ni ukiukaji wa vikwazo vya silaha ilivyowekewa nchi hiyo.
 
Korea Kaskazini imekuwa chini ya vikwazo vya Umoja wa Mataifa kwa sababu ya mipango yake ya makombora ya balestiki na ya nyuklia tangu 2006, na hatua hizo zimeimarishwa zaidi kwa miaka kadhaa sasa.
 
Kwa mujibu wa ripoti ya wataalamu hao, taarifa iliyotolewa na mamlaka ya Ukraine kuhusu mapito ya njia lilikotokea kombora hilo inaonyesha kuwa lilirushwa kutokea ndani ya eneo la ardhi ya Shirikisho la Russia.
Rais Vladimir Putin wa Russia (kulia) na Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un

Wachunguzi wa Umoja wa Mataifa wamesema, makombora hayo ya balestki aina ya Hwasong-11 yalijaribiwa hadharani na Pyongyang mnamo mwaka 2019.

 
Marekani na nchi nyingine za Magharibi zimeituhumu Korea Kaskazini kuwa imeipelekea silaha Russia za kutumia katika vita dhidi ya Ukraine, tuhuma ambazo Moscow na Pyongyang zimezikanusha licha ya kuahidi mwaka jana kuwa zitaimarisha uhusiano wao wa kijeshi.

Katika mkutano wa Baraza la Usalama wa mwezi Februari, Washington iliituhumu Moscow kuwa ilirusha mara zisizopungua tisa makombora ya balistiki ya Korea Kaskazini dhidi ya Ukraine kupitia operesheni maalumu ya kijeshi iliyoanzisha dhidi ya nchi hiyo February 2022.../

Tags