Sep 09, 2024 02:56 UTC
  • Jumatatu, 09 Septemba, 2024

Leo ni Jumatatu tarehe 05 Mfunguo Sita Rabiul Awwal 1446 Hijria sawa na tarehe 09 Septemba 2024.

Siku kama ya leo miaka 1452 iliyopita kulianza vita maarufu kwa jina la vita vya miaka saba kati ya madola mawili yaliyokuwa na nguvu ya Iran na Roma, baada ya mfalme Justinian wa Roma kuanzisha mashambulizi yaliyokuwa na lengo la kulikalia eneo la magharibi mwa Iran.

Baada ya miaka saba ya vita mfalme wa Iran Anushirvan alimshinda mfalme Justinian wa Roma na hivyo mfalme huyo akalazimika kujiuzulu. Baada ya kujiuzulu Justinian, mfalme Tiberius alishika mamlaka ya utawala wa Roma.

Vita hivyo vilimalizika mwaka 579 baada ya Waroma kukubali kuilipa Iran gharama inayofikia sarafu za dhahabu elfu 45.

Katika siku kama hii ya leo miaka 196 iliyopita alizaliwa Leo Tolstoy, mwandishi na mwanafasihi raia wa Russia.

Awali Tolstoy alijiunga na jeshi la Qaukasia na katika kipindi hiki ndipo alipoandika kitabu chake cha kwanza alichokupa jina la "Childhood". Mwandishi huyo wa Russia baadae alijiengua jeshini na kutumia muda wake wote kwa ajili ya kusoma na kuandika.

Miongoni mwa vitabu muhimu vya mwandishi Leo Tolstoy ni "Vita na Amani", "Waqazaki" na "Hadji Murad." Tolstoy alifariki dunia mwaka 1910.

Siku kama ya leo miaka 79 iliyopita yaani tarehe 9 Septemba 1945, ulitiwa saini mkataba wa kusalimu amri vikosi vya Japan vilivyokuwa vimeidhibiti na kuikalia kwa mabavu China. Kwa mujibu wa mkataba huo askari milioni moja wa Japan waliweka chini silaha zao kwa amri ya Hirohito mfalme wa wakati huo wa Japan. Kwa utaratibu huo vita vya kihistoria kati ya China na Japan vikafikia tamati.

Vita vya China na Japan

Siku kama ya leo miaka 48 iliyopita, aliaga dunia Mao Zedong kiongozi wa Uchina.

Mao Zedong alizaliwa mwaka 1893 na mwaka 1921 aliunda chama cha Kikomonisti cha Uchina baada ya kuungwa mkono na wafuasi wa fikra zake.

Mao alikuwa akisisitiza suala la kuwatetea na kuwalinda wanavijiji na kwa sababu hiyo ilipata uungaji mkono mkubwa wa wanavijiji wa Uchina.

Mao Zedong

Katika siku kama ya leo miaka 45 iliyopita yaani tarehe 19 Shahrivar aliaga dunia Sayyid Mahmoud Taleghani kiongozi wa kidini, mwanaharakati, mwanamapambano na mfasiri wa Qur'ani Tukufu wa Iran.

Ayatullah Taleghani alikuwa akifuatilia kwa karibu matukio ya kisiasa ya Iran tangu akiwa kijana. Kipindi fulani alitiwa nguvuni na kufungwa jela miaka miwili na utawala wa Kitaghuti wa Shah uliokuwa ukitawala hapa nchini kwa kosa la kushiriki katika harakati ya wananchi ya tarehe 15 Khordad.

Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu aliteuliwa na Imam Khomeini kuwa Mkuu wa Baraza la Mapinduzi na Imam wa Swala ya Ijumaa ya Tehran.

Sayyid Mahmoud Taleghani akiwa pamoja na Imam Khomeiini

 

Tags