Russia: Ulaya pia imechoshwa na siasa za ubeberu za Marekani
Waziri Mkuu wa Russia, Dmitry Medvedev amesema kuwa, nchi za Ulaya pia zimechochwa na siasa za ubeberu za Marekani.
Medvedev ameyasema hayo akiwa safarini kuelekea nchini Serbia na kuongeza kuwa, siasa za kigeni za Marekani zimejikita tu kwenye kuzingatia maslahi ya kiuchumi na kijografia ya nchi hiyo na kwamba Washington ndio mwathirika mkuu katika uga huo kutokana na tamaa yake ya kutaka kudhibiti dunia yote ikiwemo Ulaya na hasa eneo la Balkan. Waziri Mkuu wa Russia amebainisha kwamba tuhuma zinazoelekezwa na Marekani kwa serikali ya nchi hiyo au nchi nyingine pia zinatolewa kwa kuzingatia siasa mbovu za kigeni za Washington.
Dmitry Medvedev ameashiria uwepo wa Muungano wa Kijeshi wa Nchi za Magharibi NATO karibu na mipaka ya Russia na kusisitiza kuwa, takwa la muungano huo hususan Marekani la kutaka kuweka kambi zake za kijeshi karibu na mipaka ya Russia, haliwezi kuwafanya viongozi wa Moscow kutokuwa na wasi wasi na kwamba Russia itatoa jibu kali la kisiasa na kijeshi. Kadhalika ameonya juu ya hatua ya kuzishawishi nchi zilizo na tofauti za kisiasa za ndani kujiunga na Muungano wa Kijeshi wa Nchi za Magharibi NATO, na kubainisha kuwa hatua hiyo ni hatari sana kama ambavyo itakuwa na matokeo hasi.