Russia yakosoa hatua ya Marekani ya kutuma askari wengine nchini Saudia
Serikali ya Russia kupitia Wizara ya Mambo ya Nje ya nchi hiyo imekosoa vikali hatua ya Marekani ya kutuma askari wengine nchini Saudi Arabia.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kitendo hicho cha Marekani kitachochea mizozo katika eneo. Jumanne iliyopita Rais Donald Trump wa Marekani sambamba na kutuma barua kwa Baraza la Wawakilishi la nchi hiyo alidai kwamba lengo la kutumwa askari zaidi wa Marekani katika nchi hiyo ya Kiarabu ni kwa ajili ya kukabiliana na vitisho vya Iran. Itakumbukwa kuwa tarehe 14 Septemba mwaka huu kikosi cha anga cha jeshi la Yemen kwa kushirikiana na harakati ya wananchi ya Answarullah na katika kujibu jinai za muungano vamizi wa Saudia nchini humo, kilishambulia vituo vya kusafisha mafuta vya Saudia kwa kutumia ndege 10 zisizo na rubani katika maeneo ya Buqayq na Khurais.
Licha ya jeshi la Saudia lenye kumiliki mifumo kadhaa ya makombora ya Patriot iliyotengenezwa na Marekani na ambayo imesimikwa kando ya taasisi za mafuta za nchi hiyo, lakini ngao hizo hazikuweza kuzuia mashambulizi ya ndege hizo zisizo na rubani za Wayemen suala ambalo liliibua ukosoaji mkubwa wa ndani na nje ya Saudia. Hata hivyo Wamarekani na Wasaudi wameendelea kukariri madai yao yasiyo na msingi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwamba eti ndio ilihusika katika kuratibu operesheni hiyo ya ndege zisizo na rubani za Yemen dhidi ya taasisi hizo za mafuta za Saudia.