Mwanzo wa sera mpya; zawadi ya Krismasi ya Un kwa Trump
(last modified Thu, 02 Jan 2020 09:56:53 GMT )
Jan 02, 2020 09:56 UTC
  • Mwanzo wa sera mpya; zawadi ya Krismasi ya Un kwa Trump

Kiongozi wa Korea Kaskazini ameionya Marekani kuhusu sera inazofuata dhidi ya nchi yake. Kim Jong Un ametoa onyo hilo katika ujumbe wake wa mwaka mpya wa 2020 na kutangaza kuwa: "Iwapo Marekani itaendeleza siasa zake dhidi ya Korea Kaskazini, basi silaha za nyuklia kamwe hazitoangamizwa katika Rasi ya Korea."

Kiongozi wa Korea Kaskazini aidha ametangaza kuwa, kufuatia kufeli mazungumzo na Marekani kuhusu kuangamizwa silaha za nyuklia, nchi yake haifungamani tena na uamuzi wake wa kujizuia kufanya majaribio ya makombora ya nyuklia na makombora ya masafa marefu. Aidha amesema katika siku za usoni dunia itashuhudia 'silaha mpya ya kistratijia ya Korea Kaskazini'. Kiongozi wa Korea Kaskaizni amebaini kuwa, usalama wa muda mrefu wa nchi yake utadhaminiwa kwa kuwa katika hali ya tahadhari sambamba na kuwa na uwezo wa nyuklia unaoweza kukabiliana na vitisho vya Marekani. Un amesema Pyongyang hivi sasa ina mpango wa silaha mpya za kistratijia ambazo itazitumia katika makabiliano na Marekani.

Wakati huo huo, shirika rasmi la habari la Korea Kaskazini, KCNA, limechapisha ripoti iliyotangaza kuwa, Kim Jong Un amefutilia mbali muhula wa kisheria ambao nchi yake ilikuwa imetoa kwa Marekani kuhusu kufanyika mazungumzo ya nyuklia. Mbali na hayo, Kiongozi wa Korea Kaskazini amesema iwapo Marekani itaendelea kufanya mazoezi ya kijeshi katika Rasi ya Korea, basi Korea Kaskazini haitajizuia kufanya majaribio ya makombora ya balistiki ya nyuklia yenye uwezo wa kuruka baina ya mabara. 

Hotuba ya mwaka mpya ya Kim Jong Un inaonyesha kuwa, Korea Kaskazini imebadilisha sera na mitazamo yake kuhusu Marekani. Kuhusiana na hilo tunaweza kuashiria nukta kadhaa muhimu hapa.

Kwanza kabisa, weledi wa mambo ya kisiasa wanaamini kuwa, sera mpya za Korea Kaskazini  zinaashiria kumalizika udiplomasia wa miaka miwili baina ya Kim Jon Un na Donald Trump. Hapo kabla wakuu wa Korea Kaskazini walikuwa wameionya Marekani kuwa, iwapo haitakuwa imechukua hatua za kuanzisha tena mazungumzo kabla ya kumalizika mwaka 2019, basi wataipa Washington, 'zawadi ya Krismasi'.

Nukta ya pili ni kuwa,  hadi sasa kumefanyika duru tatu za mazungumzo baina ya Rais Trump wa Marekani na Kim Jong Un, Kiongozi wa Korea Kaskazini. Mazungumzo hayo yamefanyika huko Singapore, Vietnam na mpaka wa Korea mbili. Mazungumzo baina ya viongozi hao wawili yamegonga mwamba kwa sababau Marekani imekataa kutekeleza ahadi ilizotoa kwa Korea Kaskazini. Ni kwa sababu hii ndio Kiongozi wa Korea Kaskazini katika mkutano na wanachama wa chama tawala nchini humo akayataja matakwa ya Trump kuwa sawa na yale ya wahuni au magenge ya wezi. Kwa maneneo mengine ni kuwa,  wakuu wa Marekani kwa miongo kadhaa wamekuwa wakiisisitizia Korea Kaskazini kuwa, kusimamisha mpango wake wa kuunda silaha za nyuklia ni jambo litakalopelekea nchi hiyo kustawi, lakini ilipofika wakati wa kuzingatia maslahi ya kiuchumi ya Pyongyang, Marekani imekataa kutekeleza kivitendo ahadi zake.

Nukta nyingine muhimu ni kuwa, katika hali ambayo katika kipindi cha takribani miaka miwili ambayo Korea Kaskazini imejizuia kufanyia majaribio ya nyuklia makombora yake ya balistiki yenye uwezo wa kuruka mabara, Marekani imeiwekea nchi hiyo vikwazo na mashinikizo makubwa ya kiuchumi. Hivi sasa imewabainikia wakuu wa Korea Kaskazini kuwa, Marekani imekiuka ahadi ilizotoa katika mazungumzo na haijachukua hatua yoyote kwa maslahi ya Korea Kaskazini.

Kim Jong Un ametaka sasa kuchukuliwe hatua imara za kudhamini usalama wa Korea Kaskazini. Baada ya kumalizika muhula wa Pyongyang kwa Washington kuhusu mazungumzo, ujumbe wa hivi karibuni wa Kim Jong Un unaashiria kufika ukingoni muda wa kusitisha majaribio ya nyuklia ya makombora ya balistiki ya nchi hiyo.

Kiongozi wa Korea Kaskazini akiwa na wanajeshi wa nchi hiyo

Katika kipindi cha miezi 20 iliyopita, Trump na Un wamekutana mara tatu. Katika kipindi hicho, Korea Kaskazini imechukua hatua kadhaa za kistratijia ikiwa ni pamoja na kusimamisha mpango wake wa silha za nyuklia. Lakini mkabala wa hilo badala ya kuchukua hatua za  kuzingatia matakwa ya kiuchumi ya Korea Kaskazini, Marekani imeibua masharti mapya na kusema lazima Korea Kaskazini ikabidhi silaha za nyuklia, takwa ambalo limepingwa na wakuu wa Pyongyang.

Hali kadhalika Korea Kaskazini inasema wakati iliposimamisha majaribio ya makombora yake na ya silaha za nyuklia, katika upande wa pili Marekani ilitekeleza mazoezi kadhaa ya kijeshi na Korea Kusini.

Huku hayo yakijiri China na Russia zinasisitiza kuwa lazima vikwazo dhidi ya Korea Kaskazini viondolewe ili amani ya kudumu ipatikane katika Rasi ya Korea. Nayo Korea Kusini pamoja na kuwa inafuata sera za Marekani lakini imesisitiza kuwa lazima maslahi ya kiuchumi ya Korea Kaskazini yazingatiwe. 

Wakuu wa Korea Kaskazini wameamua kubadilisha sera zao kuhusu Marekani baada ya Washington kushindwa kutekelekeza ahadi ilizotoa. Weledi wa mambo wanaamini kuwa, kuongezeka taharuki baina ya Marekani na Korea Kaskazini, kutapelekea Un kuharakisha mchakato wa kufanyia majaribio makombora ya baina ya mabara yenye uwezo wa kusheheni silaha za nyuklia. 

Tags