Maelfu ya Waislamu nchini India waandamana kulaani kuuliwa shahidi Qassem Soleimani
Maelfu ya Waislamu nchini India wamelaani vikali kitendo cha Marekani cha kumuua kigaidi Jenerali Qassem Soleimani, Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran IRGC.
Kufuatia kitendo hicho cha kinyama maelfu ya Waislamu katika miji tofauti nchini India ukiwemo mji wa Bengaluru wamefanya maandamano makubwa sambamba na kupiga nara dhidi ya Marekani na kuitaka Washington kukomesha jinai zake katika eneo hili. Hii ni katika hali ambayo maelfu ya Waislamu wa eneo la Kashmir linalodhibitiwa na India hapo jana pia walimiminika katika barabara za eneo hilo wakiomboleza kifo cha Jenerali Qassem Soleimani sambamba na kuonyesha hasira zao kutokana na ugaidi wa Marekani.

Waislamu hao wa Kashmir walibeba mabango yaliyokuwa na jumbe zinazosema 'Mauti kwa Marekani, Mauti kwa Israel.' Jenerali Qassem Soleimani, Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran IRGC pamoja na Abu Mahdi al Muhandes, Naibu Kiongozi Mkuu wa Harakati ya Wananchi ya Hashdu sh-Shaabi ya Iraq, waliuawa shahidi asubuhi ya Ijumaa kupitia shambulio la kigaidi lililofanywa na kikosi cha anga cha Marekani katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa mjini Baghdad.