Kumbukumbu Maalumu ya Kuuawa Shahidi Jenerali Haj Qassem Soleimani
https://parstoday.ir/sw/news/event-i135320-kumbukumbu_maalumu_ya_kuuawa_shahidi_jenerali_haj_qassem_soleimani
Hamjambo na karibuni kuwa nasi katika kipindi hiki maalumu kinachokujieni kwa mnasaba wa kumbukumbu ya kuuliwa shahidi Meja Jenerali Qassim Soleimani.
(last modified 2026-01-19T11:38:37+00:00 )
Jan 10, 2026 07:33 UTC
  • Shahidi Haj Qassem Soleimani
    Shahidi Haj Qassem Soleimani

Hamjambo na karibuni kuwa nasi katika kipindi hiki maalumu kinachokujieni kwa mnasaba wa kumbukumbu ya kuuliwa shahidi Meja Jenerali Qassim Soleimani.

Katika kipindi hiki, tunazungumzia hadithi ya maisha na kifo cha shahidi "Mwanaume wa Iran" ambaye alisimama kidete na kishujaa kupambana na adui kwa ari ya kitaifa, ujasiri wa hali ya juu, na imani thabiti. 

Kumbukumbu ya mauaji ya Shahidi Haj Qassem Soleimani mwaka huu imesadifiana na tarehe 13 Rajab, siku ya kumbukumbu ya kuzaliwa Amiri na Kiongozi wa Waumini, Imam Ali bin Abi Twalib (AS), ambaye Mtume Muhammad (SAW) alimwita kuwa ni ndugu yake kisha akasema: "Mimi na Ali ni baba wa umma wa Kiislamu."

Wairani huadhimisha siku ya tarehe 13 Rajab, siku ya kuzaliwa Imam Ali bin Abi Twalib kuwa ni Siku ya Baba.

Qassem Soleimani pia alikuwa baba, lakini si kwa watoto wake wa kuzaa tu, bali alikuwa baba kwa kila mtu aliyekandamizwa na kudhulumiwa ambaye alisikia kilio chake cha kudai haki. Alijitambua kama askari wa Imam Ali Khamenei na alikuwa amejifunza tabia na mienendo ya ubaba kutoka kwake. Daima alikuwa akifanya jitihada za kushughulikia masuala ya watu na alijipamba kwa sifa hiyo akiwa bado mdogo.

Qassem Soleimani alizaliwa katika kijiji cha Qanat-e-Malek, katika familia ya wafugaji, ambao maisha yao yalikuwa magumu kutokana na mabadiliko ya misimu na uhamiaji. Alifanya kazi shambani tangu akiwa mdogo, huku akihudhuria masomo shuleni. Miaka hiyo, maisha yalikuwa magumu sana kwa wengi, mkate wa ngano ulikuwa haba, na watu waliishi kwa kutumia mkate wa shayiri na mtama. Kulikuwapo majira ambapo chakula pekee cha familia kilikuwa mboga mboga za nyandani.

Katika mojawapo ya miaka hiyo, aliposikia kwamba baba yake anadaiwa pesa na Benki ya Ushirika Vijijini na kwamba huenda akafungwa jela, aliamua kuchukua hatua ya kumnusuru baba yake. Akiwa na umri wa miaka 13, kijana Qassem alienda Kerman kufanya kazi kama kibarua ili aweze kulipa deni la baba yake. Lakini mwili wake mdogo uliwazuia wengi kumkubali na kumwajiri. Baada ya siku na juhudi nyingi, hatimaye alipata kazi ya kibarua katika jengo ambalo lilikuwa halijakamilika.

Miezi michache baadaye, alikuwa mfanyakazi wa hoteli. Alifanya kazi kwa miezi mitano na akatuma mshahara wake wote, ambao ulikuwa Tomani elfu moja kwa baba yake. Alitekeleza majukumu ya baba kwa baba yake mwenyewe.

Kaka yake, Sohrab Soleimani, anasimulia uhusiano wake wa karibu na familia akisema: Licha ya kulazimika kuhamia mjini kwa ajili ya kazi, Qassem alikuwa akienda kutembelea familia yake kila alipopata nafasi. Sohrab anasema kuhusu upendo wa Qassem kwa familia yake kwamba: "Mara zote alipofika nyumbani alibusu mikono ya baba na miguu ya mama. Alikuwa akisema "dua na maombi yao yanazidisha baraka katika riziki yangu."

Sifa nyingine ya Qassem Soleimani ilikuwa ujasiri na ushujaa wake mkubwa, ambao yeye mwenyewe ameusimulia katika kumbukumbu zake binafsi. Anasema: Nilikuwa na umri wa miaka kumi. Ilikuwa majira ya joto na wakati wa mavuno. Baba yangu alikuwa na fahali hatari ambaye kila mtu aliogopa asimpige pembe. Lakini mimi nilimpanda na nikamwendesha kilomita 15 hadi nyumbani kwa shangazi yangu. Ng'ombe huyo alikuwa akikataa kutii; aligonga kichwa chake kwenye miguu yangu. Lakini mimi, niliendelea na safari yangu kupitia nyandani.... Haj Qassem anasisitiza kwamba "tangu utotoni, sikuwa na hofu hata kidogo."     *******

Asubuhi ya Januari 3, 2020, hali ya hewa ya majira ya baridi kali ilihinikiza kote. Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Baghdad ulikuwa ukiendelea na shughuli zake nyingi kama usiku mwingine; ndege zilikuwa zikitua na kuondoka, teksi zilikuwa zikipita barabarani kuelekea na kutoka jijini, na kwa watu wengi, ilionekana kama usiku wa kawaida. Lakini nyuma ya utulivu huo wa kidhahiri tu, hadithi nyingine ilikuwa ikiendelea. Qassem Soleimani, ambaye aliongoza Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa miaka mingi, aliwasili Baghdad kwa mwaliko rasmi wa serikali ya Iraq. Alikwenda Iraq akitokea Damascus, njia ambayo alikuwa ameizoea sana katika kipindi chote cha mapambano dhidi ya kundi la ISIS.

Kwa upande mwingine, mwenyeji wake, Abu Mahdi al-Muhandis, aliyekuwa Naibu Mkuu wa Kikosi cha Uhamasishaji cha Wananchi wa Iraq, Al Hashdul Shaabi, kiongozi wa Kataib Hizbullah, na mtu aliyekuwa na ushawishi mkubwa katika milinganyo ya usalama ya Iraq, alikwenda uwanjani kumkaribisha. Abu Mahdi alikuwa na nafasi na mchango mkubwa na muhimu katika miaka ya mapambano na kundi la kigaidi la Daesh akishirikiana na vikosi vya jeshi la Iraq na washirika wao wa kikanda.

Abu Mahdi al Muhandes 

Ndege iliyokuwa imembeba Haj Qassem ilitua kwenye uwanja wa ndege wa Baghdad. Kwa watu wengi waliokuwa uwanjani hapo, huko kulikuwa kutua kwa ndege ya kawaida; lakini kwa wanajeshi wa Marekani, ulikuwa mwanzo wa operesheni ya siri ya mauaji makubwa. 

Baada ya kuteremka, Haj Qassem Soleimani na wenzake walipanda magari kadhaa kutoka nje ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Baghdad. Wakati huo huo, ndege zisizo na rubani za Marekani zilikuwa zikifuatilia mwendo wa msafara huo zikiwa na taarifa kamili tangu ndege hiyo ilipotua.

Dakika chache baadaye, wakati msafara huo ulipokuwa barabarani kuondoka uwanja wa ndege, milio ya mabomu ilivunja ukimya wa usiku wa manane wa mji Baghdad. Magari ya msafara huo yalishika moto, na katika muda mfupi sana, habari za mlipuko mkubwa zilienea kati ya watu wa Baghdad. Dakika chache baadaye, vyombo vya habari vilitoa ripoti isiyo rasmi kuhusu tukio hilo, kisha vilinukuu vyanzo mbalimbali, kwamba shabaha ya shambulio hilo ilikuwa msafara uliokuwa na Haj Qassem Soleimani na Abu Mahdi al-Muhandis.. Saa chache baadaye, Wizara ya Ulinzi ya Marekani ilitangaza rasmi kwamba shambulio hilo lilifanywa kwa amri ya moja kwa moja ya Rais wa nchi hiyo; kitendo ambacho kilionekana kuanzia saa za awali kabisa za tukio hilo kuwa ni mauaji ya "kigaidi."

Kuanzia wakati huo na kuendelea, kilichotokea hakikuwa tena "tukio la kijeshi" pekee; bali lilikuwa shambulio la moja kwa moja dhidi ya mamlaka ya kitaifa ya Iran na ukiukaji dhahiri wa sheria za kimataifa. Nchini Iraq pia, majadiliano kuhusu "mamlaka ya kitaifa" na "nafasi ya vikosi vya majeshi ya kigeni" katika ardhi ya nchi hiyo yalirudi tena katika uwanja wa siasa; na duniani kote, wachambuzi walikariri swali moja: Shambulio hili linalipeleka eneo hilo katika mwelekeo gani?

Asubuhi ya siku iliyofuata, Wamarekani walidhani walikuwa wametekeleza mauaji kwa mafanikio, na kwamba kwa kufanya hivyo, wamepunguza ushawishi na nafasi ya Iran katika eneo la Asia Magharibi. Hata hivyo, katika siku zilizofuata, mahudhurio makubwa ya wananchi kwenye mitaa ya miji mbalimbali ya Iran yalibadilisha kabisa taswira hiyo. Mazishi na shughuli za maombolezo makumbwa zilifanyika katika miji mikubwa na midogo kote nchini. Hali hiyo ilishuhudiwa pia katika nchi za Iraq, Syria, Lebanon, India, Pakistan, na hata baadhi ya nchi za Ulaya.

Picha za umati mkubwa wa watu kwenye mazishi ya mashahidi nchini Iran zilionekana kwenye televisheni na mitandao ya kijamii. Mashirika ya habari yaliandika kwamba, maombolezo makubwa kama hayo hayajawahi kuonekana popote duniani tangu baada ya mazishi ya Imam Ruhullah Khomeini (RA). Kwa sehemu kubwa ya jamii ya Iran na watu wa eneo la Magharibi mwa Asia, Kamanda Soleimani alikuwa nembo ya Muqawama na mapambano; mtu ambaye uwepo wake nchini Syria, Iraq, na sehemu zingine za eneo Asia Magharibi ulikuwa tumaini kwa watu kupata amani na utulivu.   

Imam Ruhullah Khomeini (M.A)

Shughuli ya maombolezo na mazishi ya Kamanda Soleimani na wenzake haikuwa ya kidini au kitaifa tu; bali ilikuwa onyesho la pamoja la hisia, utambulisho na mshikamano wa kikanda. Watumiaji wengi wa mitandao ya kijamii katika nchi mbalimbali kama Iran, Iraq, Lebanon, Pakistan, Syria, India na kadhalika walimtaja Soleimani kwa kutumia hashtag na picha mbalimbali, wakimwita "shujaa" au "mlinzi wa watu wa eneo la Asia dhidi ya magaidi wa ISIS."

Katika mazingira kama hayo, dhana nyingine iliibuka polepole; dhana ambayo ilizidi upeo wa mtu binafsi na kutaja seti ya mienendo, imani, na mitindo ya maisha kama "Shule ya Soleimani." Istilahi hii, polepole ilienda mbali na tafsiri ya kihisia na kuwa mjadala wa kisiasa na kitamaduni.

Istilahi ya "Shule au Mfumo wa Soleimani" haikuwa na maana ya rekodi ya kijeshi pekee, bali aina ya masuala ya kiroho yaliyoandamana na mfungamano na maadili ya Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran. Shule hii ina upeo mpana zaidi ya taifa na umeenea katika kanda nzima na Mhimili wa Muqawama. Inatilia mkazo kuisha maisha ya kujiepusha na anasa, kujitenga na upendeleo wa kiuchumi na kirasmi, na kuwa tayari kwenda mstari wa mbele wa mapambano" kwa maana halisi ya neno hilo.

Katika shule hii, Soleimani anatambulishwa si kama kamanda kwenye uwanja wa vita tu, bali pia kama mfano na kigezo cha kuigwa katika masuala mengi; Haj Soleimani anatambulishwa kama mtu anayeshiriki kikamilifu katika medani za kijeshi, mwenye mchango muhimu katika siasa za kikanda, na baba mwenye uhusiano mwema na wa kihisia na familia za wapiganaji katika medani za vita. Zaidi ya haya yote ni kwamba, Haj Qassem alitambuliwa kuwa mtu aliyekuwa na nafasi ya aina yake katika kukabiliana na migogoro ya kijamii. "Shule ya Soleimani" ni wito wa "kujitolea kwenye medani zinazovuka mipaka ya kijiografia” na kutetea makundi na jamii yanayohisi kuwa chini ya mashinikizo, dhulma, uvamizi, au ubaguzi. 

Haj Qassem anaeleza kujitolea huko katika barua aliyomwandikia binti yake akisema: "Ninajiona kama askari anayesimama mbele ya mlango wa kila Muislamu aliye hatarini, na namuomba Mungu anipe nguvu ya kuwatetea watu wote wanaokandamizwa duniani. Niko tayari kufa, si kwa ajili ya Uislamu azizi tu, ambao roho yangu si chochote wala lolote mbele yake; si kwa ajili ya Shia wanaokandamizwa tu, bali kwa ajili ya mtoto mwenye hofu, asiyejiweza, ambaye hakuna pa kukimbilia. Ninampigania mwanamke anayepakata mtoto kifuani mwake kwa hofu, na mkimbizi anayekuwa mbioni akifukuzwa, na kuacha alama ya damu nyuma yake.”

Wanaume wengi walisoma na kuhitimu katika shule ya Soleimani, wengi wao hatuwajui. Mmoja wao alikuwa Shahidi Tehrani Moghadam, ambaye, kutokana na bidii, istiqama, elimu na maarifa, aliweza kuifikisha Iran kwenye vilele vya juu vya sayansi na elimu katika uwanja wa taaluma ya masuala ya anga za mbali. Watu kama Mohsen Fakhrizadeh, Kamanda Hossein Salami, Amir Ali Hajizadeh, Hossein Bagheri, na kadhalika, wote walihitimu katika shule na maktaba ya Haj Qassem Soleimani.

Ingawa baadhi ya wasomi na makanda hao waliuawa katika vita vya siku 12 vya utawala wa Kizayuni na Marekani dhidi ya Taifa la Iran, lakini hapana shaka kuwa Shule ya Soleimani bado ina wahitimu wengi ambao tutakuja kuwajua vyema katika siku zijazo.