B’Tselem: Wapalestina wasiopungua 84 wameuawa kwenye kambi za mateso za Israel
Mfumo wa magereza wa utawala wa kizayuni wa Israel umekuwa "mtandao wa kambi za mateso" unaowalenga Wapalestina. Hayo yameelezwa katika ripoti mpya ya uchunguzi uliofanywa na asasi ya kutetea haki za binadamu ya B'Tselem.
Ripoti hiyo inabainisha kwa kina unyanyasaji wenye wigo mpana, vifo vinavyotokea wakati Wapalestina wakiwa kizuizini na kile ambacho asasi hiyo kutetea haki za binadamu ya Israel imekielezea kama sera ya makusudi ya serikali ya kufanya ukatili.
B'Tselem imeeleza katika ripoti hiyo iliyotolewa jana Jumanne kwamba, tangu Oktoba 2023 hadi sasa, Wapalestina wasiopungua 84, akiwemo mtoto mmoja, wamefia kwenye vituo vya kizuizi vya Israel.
Asasi hiyo imetanabahisha kwamba idadi halisi inaweza kuwa kubwa zaidi, kwa sababu kesi nyingi kuhusiana na vifo hivyo bado hazijathibitishwa au zimefichwa.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Wapalestina 50 kati ya waliouawa ni kutoka Ukanda wa Ghaza, 31 Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu na watatu ni Wapalestina raia wa Israel.
Halikadhalika, shirika hilo la kutetea haki za binadamu limeeleza kwamba, hadi kufikia Januari 2026 mamlaka za utawala wa kizayuni wa Israel zimekuwa zikiendelea kuishikilia miili ya Wapalestina 80 na kukataa kuirudisha kwa familia zao.
Ushuhuda uliokusanywa kutoka kwa Wapalestina waliokuwa kizuizini unaelezea kile asasi hiyo imekiita unyanyasaji wa kimfumo ulioko katika mfumo mzima wa magereza ya Israel.
Njia za mateso zilizoorodheshwa ni pamoja na "unyanyasaji wa kimfumo, ikiwa ni pamoja na ukatili wa kimwili na wa kisaikolojia, mazingira yasiyo ya kibinadamu wanayoishi Wapalestina, kuwekwa na njaa kwa makusudi na kunyimwa matibabu".
Wapalestina kadhaa waliowahi kushikiliwa kwenye magereza ya utawala wa kizayuni wamesimulia kwamba walifanyiwa au walishuhudia, udhalilishaji wa kingono wakati walipokuwa kizuizini.../