Jan 03, 2026 10:46 UTC
  • Leo katika historia
    Leo katika historia

Leo ni Jumamosi 13 ya mwezi Rajab 1447 Hijria mwafaka na 3 Januari 2026 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1470 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, alizaliwa katika nyumba tukufu ya al Kaaba, Ali bin Abi Twalib AS, ambaye ni binamu, mkwe na Khalifa wa Mtume Muhammad (saw). Mama wa mtukufu huyo ni Bibi Fatima bint Assad na baba yake ni Abu Talib. Katika kipindi chake cha utotoni, Ali bin Abi Talib alilelewa na kupata elimu na mafunzo kutoka kwa Mtume Mtukufu SAW, na alikuwa mwanaume wa kwanza kuukubali Uislamu. Mwishoni mwa mwaka wa Pili Hijria, Imam Ali AS alimuoa Bibi Fatimatul Zahra binti ya Mtume Mtukufu SAW. Imam Ali AS alishiriki kwenye vita vyote bega kwa bega na Mtume Mtukufu SAW isipokuwa vita vya Tabuk, na alikuwa msaidizi wa karibu wa Mtume katika hali zote za shida na matatizo. Licha ya kuwa shujaa na mpiganaji asiye na mithili, lakini Imam Ali bin Abi Talib alikuwa mpole, mwingi wa huruma na mtetezi wa wanyonge.

 

Leo tarehe 13 Rajab zinaanza siku zinazojulikana katika dini kuwa ni "Siku Nyeupe" au siku za ibada ya Itikafu ambazo ni siku za tarehe 13, 14 na 15 za mwezi huu wa Rajab. Katika siku hizi waumini wanashauriwa kufanya ibada ya itikafu ya kukaa na kubaki katika sehemu au mahala maalumu hususan misikitini na maeneo matakatifu kwa ajili ya ibada na kumdhukuru Mwenyezi Mungu SW. Watu wanaofanya itikafu hutakiwa kufunga Saumu siku tatu mfululizo wakiwa katika jitihada za kuondoka katika minyororo ya dunia hii finyu na kujikuribisha kwa Allah. Ibada ya itikafu imehimizwa sana na Mtume Muhammad (saw) na maimamu watoharifu katika kizazi chake.

 

Katika siku kama ya leo miaka 1168 iliyopita yaani sawa na tarehe 13 Rajab mwaka 279 Hijria, alifariki dunia Abu Isa Tirmidhi hafidh wa Qur'ani Tukufu na mpokeaji hadithi mashuhuri wa Kiislamu. Tirmidhi alifanya safari katika nchi mbalimbali kwa miaka mingi kwa ajili ya kujipatia elimu ya dini na hadithi. Alikuwa miongoni mwa wanafunnzi hodari wa Imam Bukharin na kitabu chake maarufu zaidi ni Swahih Tirmidhi. Kitabu hicho kinahesabiwa kuwa miongoni mwa marejeo muhimu ya hadithi katika madhehebu ya Suni. Aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 70.

 

Siku kama ya leo miaka 37 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 13 Dei 1367 Hijria Shamsia, ujumbe wa Imam Ruhullah Khomeini, mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran uliwasilishwa kwa Mikhail Gorbachev kiongozi wa mwisho wa Umoja wa Kisovieti akimlingania dini ya Kiislamu na kumtaka aachane na fikra za Kimaksi. Katika sehemu moja ya ujumbe huo Imam Khomeini alisema: "Tatizo kuu la nchi yako si suala la umiliki, uchumi wala uhuru, bali ni kutokuwa na imani ya kweli juu ya Mwenyezi Mungu; na tatizo hilo ndilo lililoitumbukiza au litakaloitumbukiza Magharibi katika mporomoko wa kimaadili na kuifanya igonge ukuta. Tatizo lenu kubwa ni kupigana vita visivyokuwa na faida dhidi ya Mwenyezi Mungu." Mwishoni mwa ujumbe huo Imam Khomeini alisema: "Tokea sasa Ukomonisti unapaswa kutafutwa kwenye majumba ya makumbusho ya kisiasa duniani; kwani hauwezi kukidhi mahitaji halisi ya mwanadamu." Imam Khomeini alimuusia Gorbachev akisema: "Nakutaka ufanye uchunguzi wa kina kuhusu Uislamu, sio kwa sababu Uislamu na Waislamu wanakuhitajia wewe, hapana, bali kutokana na thamani za hali ya juu na za ulimwengu mzima za dini hiyo ambayo inaweza kuwa wenzo wa ufanisi na uokovu wa mataifa mbalimbali na kukidhi matatizo makubwa ya mwanadamu." 

 

Katika siku kama ya leo miaka 33 iliyopita, inayosadifiana na Januari 3, 1993 kulitiwa saini makubaliano ya Start-2 kati ya Marais wa zamani wa Russia na Marekani, Boris Yeltsin na Bill Clinton. Kwa mujibu wa makubaliano hayo, nchi hizo mbili zinapaswa kupunguza theluthi mbili za silaha zao za nyuklia. Makubaliano ya Start-1 yenye lengo hilohilo yalitiwa saini mwaka 1987 kati ya Marais Mikhael Gorbachev wa Russia na Ronald Reagan wa Marekani. Hata hivyo badala ya kuanza kuharibu silaha zake za nyuklia, Marekani ilijilimbikizia sialaha zaidi za aina hiyo suala ambalo liliilazimisha pia Russia kusitisha mpango wa kuanza kuharibu silaha zake za atomiki.

 

Na miaka 6 iliyopita katika siku kama ya leo, Luteni Jenerali Qassem Suleimani, Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, aliuawa shahidi katika shambulio la anga lililofanywa na jeshi vamizi na la kigaidi la Marekani karibu na uwanja wa ndege wa Baghdad nchini Iraq kwa amri ya moja kwa moja ya Rais Donald Trump wa Marekani. Shahidi Qassim Suleimani alizaliwa tarehe 20 Isfand 1335 Hijria Shamsia katika mji wa Kerman.  Wakati wa utoto na kuinukia kwake aliupitisha akiwa pamoja na baba yake. Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na kuundwa Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH alijiunga na kikosi hicho. Wakati wa kuanza vita vya kulazimishwa vya miaka minane vya Iraq dhidi ya Iran, Qassim Suleimani akawa akitoa mafunzo kwa brigedi za kijeshi mjini Kerman na kuzituma katika medani ya vita. Mwaka 1360 Qassim Suleimani akateuliwa kuwa kamanda wa kikosi cha 41 cha Tharallah. Kikosi hicho chini ya uongozi w Qassim Suleimani kilitekeleza operesheni nyingi wakati wa vita vya kujihami kutakatifu kama Walfajr 8, Karbala 4, Karbala 5 na kadhalika. Mwaka 1389 akateuliwa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kuwa, Kamnada wa Kikosi cha Qusd cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH. Baada ya kuibuka kundi la kigaidi la Daesh nchini Iraq na Syria, Luteni Jenerali Qassim Suleimani alihudhuria katika medani za vita za mataifa hayo akiitikia wito wa viongozi wa nchi hizo na kuwa na nafasi kubwa katika kuliangamiza kundi hilo la kigaidi. Hatimaye aliuawa shahidi alfajiri ya kuamkia Ijumaa ya tarehe 3 Januari 2020 pamoja na Abu Mahdi al-Muhandis, aliyekuwa Naibu Mkuu wa Al-Hashdu-Sha'abi pamoja na wenzao wengine wanane katika shambulio la anga lililofanywa na jeshi vamizi na la kigaidi la Marekani kwa amri ya rais wa nchi hiyo Donald Trump.