Uchunguzi wa maoni wa CNN: Wamarekani wengi wanataka Trump atimuliwe
Matokeo ya uchunguzi mpya wa maoni yanaonyesha kuwa, Wamarekani wengi wanataka Rais Donald Trump wa nchi hiyo ahukumiwe na kuondolewa madarakani.
Matokeo ya uchunguzi huo wa maoni uliofanywa na televisheni ya CNN yanaonyesha kuwa, asilimia 51 ya Wamarekani wanataka Trump ahukumiwe na kuondolewa madarakani.
Asilimia 45 ya Wamarekani walioshiriki katika uchunguzi huo wametoa maoni tofauti, na asilimia 4 wamesema kuwa hawa maoni kuhusiana na suala hilo.
Wamarekani waliowengi wanasema kuwa, maseneta wa nchi hiyo wanapaswa kumhukumu na kumuuzulu Rais Trump katika kikao cha kumsaili kiongozi huyo.
Vilevile matokeo ya uchunguzi huo wa maoni yanaonyesha kuwa asilimia 58 ya Wamarekani wanaamini kuwa, Donald Trump ametumia vibaya madaraka yake kwa ajili ya maslahi binafsi ya kisiasa.
Ripoti ya CNN imesema kuwa, huu ndio uchunguzi wa kwanza wa maoni uliofanyika Marekani baada ya Kongresi ya nchi hiyo kutuma azimio lililopasishwa na baraza hilo la wawakilishi ikitaka Trump asailiwe na kuuzuliwa.

Juhudi mpya za kutaka kumsaili Trump zilianza baada ya kufichuliwa mazungumzo ya simu kati yake na Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine. Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika mwishoni mwa mwezi Julai mwaka jana, Trump alimtaka rais huyo wa Ukraine kumpatia taarifa ambazo zinaweza kumchafua Joe Biden, mgombea wa chama cha Democrat katika uchaguzi wa 2020 na ambaye pia ni hasimu wake mkubwa wa kisiasa.