Feb 11, 2020 12:02 UTC
  • Warohingya 16 wapoteza maisha katika ajali ya boti Bangladesh

Kwa akali Waislamu 16 wa jamii ya Rohingya wamefariki dunia baada ya boti yao kuzama katika Pwani ya Bengal, kaskazini mwa Bangladesh.

Gadi ya Pwani ya Bangladesh imesema boti hiyo ya plastiki ilikuwa imejaa kupita kiasi, kwani ilikuwa na wakimbizi 125 wa Rohingya. Wapiga mbizi wa Bangladesh wamesema boti hiyo iliyozama mapema leo Jumanne katika kisiwa cha St. Martin ilikuwa inaelekea Malaysia. 

Iqbal Hossain, afisa wa polisi katika eneo la Cox's Bazar amesema wakimbizi 62 wa Rohingya ndio wameweza kunusuriwa, na kwamba wamefanikiwa kuopoa majini miili ya wanawake 14, mtoto mmoja na mwanaume mmoja. 

Waislamu wa Myanmar wanaume kwa wanawake pamoja na watoto wadogo wamekuwa wakifariki dunia mara kwa mara katika matukio ya kuzama boti wakikimbia mauaji na ukandamizaji unaofanywa na wanajeshi wa serikali ya Myanmar dhidi ya jamii hiyo.

Wakimbizi Waislamu wa Rohingya wanakumbana na maisha ya dhiki ya ndani na nje ya nchi yao

Itakumbukwa kuwa wimbi jipya la mauaji, mashambulizi na ubakaji wa jeshi la Myanmar katika mkoa wa Rakhine kuwalenga Waislamu wa Rohingya, lilianza tarehe 25 Agosti mwaka 2017 ambapo zaidi ya Waislamu elfu sita waliuawa na wengine elfu nane kujeruhiwa. Aidha zaidi ya Waislamu wengine milioni moja wa jamii hiyo walilazimika kukimbilia nchi jirani ya Bangladesh.

Hujuma za jeshi la Myanmar kwa kushirikiana na Mabudha wenye misimamo ya kigaidi katika mkoa wa Rakhine kuwalenga Waislamu hao zilianza tangu mwaka 2012.

Tags